Mwezi uliopita, Simba ilimshusha straika anayetajwa kuwa hatari katika kufumania nyavu, Mghana, Aboagye Gerson, hata hivyo baada ya ligi kumalizika, ilidaiwa kuwa amerejea kwao, lakini imegundulika kuwa nyota huyo bado yuko Dar, lakini anashinda, analala na kufanya mazoezi na wachezaji wa Yanga.
Nyota huyo yupo Dar akiendelea kujifua kwenye uwanja uliopo maeneo jirani na Kituo cha Daladala cha Simu2000, kwa ajili ya kujiweka fiti.
Simba ndiyo inamgharimia kila kitu kwa kumtunza, ambapo inasemekana analala kwenye hoteli moja iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam.
Chanzo cha kuaminika kimesema kuwa kwa muda mrefu nyota huyo amekuwa akipasha uwanjani hapo pamoja na wachezaji wengine wa Yanga, akiwemo Kpah Sherman na nyota wa Sierra Leone, Lansana Kamara, ambaye inaelezwa ameletwa kufanya majaribio Yanga.
Nyota huyo alitua Msimbazi akitokea Klabu ya Zhakoya ya nchini Iraq, alifanya mazoezi na Simba mwishoni mwa ligi msimu uliomalizika chini ya Mserbia, Goran Kopunovic.
“Mbona yupo hapa Bongo na anafanya mazoezi na kina Sherman pale uwanja uliopo karibu na Kituo cha Simu2000 na amepangishiwa pale (anaitaja hoteli), kila wakati utamuona na wachezaji hao wa Yanga.
“Inaelezwa kuwa yeye na huyo jamaa wa Sierra Leone wanalala hoteli moja na wakati wote wamekuwa pamoja,” alisema mtoa habari wetu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alipotafutwa kutolea ufafanuzi suala hilo, alisema yuko bize na ametingwa na kazi nyingi kisha akakata simu, wakati rais Evans Aveva, simu yake haikupokelewa licha ya kupigiwa mara kadhaa.