Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili
ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa
tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, Mwananchi ilitaarifiwa wiki hii kuwa
Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili
vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na
taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa
mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato
wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya makada
wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu
ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina
Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa ambazo gazeti hili imezipata zinaeleza
kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura
ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea
baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa kundi hilo
limekuwa likifanya vikao mbalimbali vya kuweka mkakati wa jinsi gani ya
kuivuruga Kamati Kuu kabla ya kuchuja majina ya wagombea urais kwa
tiketi ya CCM.
“Kuna mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa
kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani
ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi
kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika
serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa
viongozi wa juu wa CCM.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika
kwa umakini mkubwa ili kuweza kuhakikisha Kamati Kuu haikati jina la
mgombea wa kundi hilo kama ambavyo imewahi kufanyika kwa makada wengine
ambao majina yao hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya
kupigiwa kura kutokana na nguvu yao kwenye chama.
Kama hilo litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili
kutokea baada ya mwaka 1995, Jakaya Kikwete kumlalamikia aliyekuwa
katibu mkuu wa CCM, Lawrance Gama kuwa hawezi kumtendea haki baada ya
kuonekana akiwa amevaa nguo yenye nembo ya mmoja wa waliokuwa wakiwania
kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
Alipoulizwa kuhusu mkakati huo, katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa wamesikia na kuelezwa kuwa
kundi hilo linagawa fedha kufanikisha jambo hilo kwa kuwa wanadhani
sekretarieti ya chama haiwapendelei wao.
“Wanadhani kuna watu wanapendelewa, kama suala
hilo lipo bila shaka chama hakiwezi kukaa kimya kwani huo ni uasi na
usaliti kwa chama,” alisema Nape.
Alisema kuwa ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye mikutano sahihi ya chama.