MGANGA mmoja wa kienyeji amekamatwa akifanya ushirikina katika Mahakama ya wilaya ya Bunda mkoani Mara kwa kutumia tunguli ili kuwezesha kushinda kesi.
Mganga huyo ni moja kati ya waganga sita, ambao walikamatwa kwa kosa
la kupiga ramli chonganishi na kufunguliwa kesi katika mahakama hiyo ya
wilaya.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walikamatwa Machi 11 mwaka huu
saa 6:00 mchana katika kijiji cha Kabasa wilayani hapa, wakipiga ramli
chonganishi ya kuchonganisha wananchi kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa huyo aliyeshikwa juzi akifanya ushirikina huo katika
mahakama hiyo ni Riku Wasaga Yahaya (50), mkazi wa kijiji cha Kabasa
wilayani hapa.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walipokamatwa wakipiga ramli
chonganishi, walifunguliwa kesi namba 86 ya mwaka huu katika mahakama
hiyo.
Mwendesha mashitaka wa Polisi, Athumani Salum, alidai kuwa juzi
wakati watuhumiwa hao wakiwa mahakamani hapo, wakisubiri kesi yao
kutajwa, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso, mtuhumiwa
Yahaya alionekana akifanya ushirikina kwa kutumia tunguli.
Ilidaiwa baada ya mtuhumiwa huyo kupekuliwa na polisi, walimkuta
akiwa na vibuyu viwili vya tunguli na dawa ya ungaunga na mchanga
mfukoni mwake, alivyokuwa anavitumia kufanyia ushirikina katika mahakama
hiyo.
Hakimu Kasonso alisema mtuhumiwa huyo na wenzake watano, walikamatwa
wakijaribu kufanya ushirikina wa kuroga mahakama hiyo, jambo ambalo ni
la ajabu mno, kwani Mahakama ni chombo ambacho kazi yake ni kutoa haki
na kutafsiri sheria kikamilifu na kwa kina zaidi ili haki iweze
kutendeka.
Hakimu Kasonso alisema kuwa kitendo hicho cha ushirikina ndani ya
chombo cha haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa na hivyo mahakama hiyo
inawapeleka mahabusu watuhumiwa wote sita kwa muda wa siku 14 hadi Mei
22, mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.
"Mahakama ni chombo cha kisheria ambacho kinatoa haki baada ya
kuitafsiri sheria kwa kina zaidi na kisha kutoa maamuzi, sasa kitendo
cha kuja kufanya ushirikina katika chombo ambacho kazi yake ni kutenda
na kutoa haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa, hivyo watuhumiwa wote waende
mahabusu siku 14," alisema.
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Athuman Salum, aliwataja
watuhumiwa wengine katika ile kesi yao ya awali ya kupiga ramli
chonganishi kuwa ni Komoga Wasaga Msiba, Thomas Nyakojaribu, Oro Odewa
Kalidoshi, Mariamu Thomas na Daud Thomas, wote ni wakazi wa kijiji cha
Kabasa wilayani Bunda.