Dar na Z’bar. Vikao vya Kamati Kuu ya CCM na Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar vinaonekana kuwa huenda vikaiweka hadharani siri nzito za urais wa Jamhuri ya Muungano.
Mkutano wa sekretarieti ndiyo utakaoanza leo
ukifuatiwa na Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar huku Kamati Kuu ya CCM
ikitarajiwa kukutana Jumanne wiki ijayo katika Ofisi Kuu ya CCM
Kisiwandui kujadili na kutathmini hali ya kisasa kuelekea Uchaguzi Mkuu
mwaka huu.
Kikao hicho kimekuja huku wagombea wa nafasi ya
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho wakipishana
kwa usafiri wa ndege na boti kwenda Zanzibar kutafutwa kuungwa mkono na
wajumbe wa NEC na waliopo visiwani humo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alithibitisha kikao hicho kufanyika Zanzibar na kitaoongozwa na
Mwenyekiti wake Rais Dk Jakaya Kikwete ambaye amebakisha muda mfupi
kumaliza muhula wake wa uongozi tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Vuai alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana, itatanguliwa na Kikao cha Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar.
Alisema suala kubwa ambalo watalijadili ni
kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010/2015 tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Hata hivyo, Vuai alisema hayuko tayari kuzungumzia
ajenda ya kikao cha Kamati Kuu kwa vile majukumu hayo yako kwa Katibu
wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye.
Pia, alisema Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar
itakuwa na ajenda ya mengineyo itakayojadili hali ya kisiasa tangu
kumalizika uchaguzi mkuu uliopita ambapo kikao hicho tayari matayarisho
yake yamekamilika kabla ya kuanza kamati Kuu kukutana visiwani humu.
Nape
Hata hivyo, Nape alisema jana kuwa Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya CCM, inakutana leo jijini Dar es Salaam kupanga
ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya Taifa ya chama hicho itakayokutana Zanzibar Jumanne ijayo.
Alisema kuwa kikao hicho ni cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete.
Kikao cha Kamati Kuu kinakutana na kukiwa na
patashika ya makada wa CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya urais
wakipishana kwa safari za usafiri wa majini na angani na wapambe wao
kukutana na wajumbe wa NEC na mkutano mkuu katika vikao vya faragha
Pemba na Unguja kuomba ushawishi wa kuungwa mkono.