MASHOGA kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki wamekutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam, zinasema mashoga hao
walikutana juzi katika Ukumbi wa Kivukoni 3 ulioko katika Hoteli ya
Serena na kuwashirikisha wasichana wanaofanya mapenzi kinyume na
maumbile.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mashoga hao wapatao 50 walitoka katika nchi za Kenya na Uganda na waliungana na wenzao wa Tanzania.
Mwandishi wa MTANZANIA aliyepata taarifa za uwepo wa mkutano huo,
alishuhudia jinsi mkutano huo ulivyokuwa ukiendeshwa kwa usiri wa hali
ya juu kwa kuwa kila aliyekuwa akitaka kuingia ukumbini alikuwa
akizuiwa.
Pamoja na watu wasiohusika kutotakiwa kuingia ukumbini, hata wahudumu wa
hoteli hiyo walikuwa wakiruhusiwa kuingia ukumbini kwa tahadhari ili
wasijue kinachoendelea.
Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, mashoga hao walikuwa wakisitisha
mjadala kila wahudumu walipokuwa wakiingia ukumbini kwa ajili ya kutoa
huduma na mazungumzo yalikuwa yakiendelea baada ya wahudumu kutoka
ukumbini.
Pamoja na ulinzi uliokuwa mahali hapo, taarifa zilisema mada kuu
iliyowakutanisha mashoga hao ilikuwa ni kujadili changamoto
zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi. Pia taarifa zinasema
walikuwa wakijadili namna ya kufanya utafiti wa kukabiliana na
changamoto hizo.
Pamoja na mashoga hao kuonyesha walikuwa wakijadili masuala ya afya ya
kimataifa, Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris
Mwamwaja, alisema wizara hiyo haikuwa na taarifa za mkutano huo.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania ushoga hauruhusiwi lakini wiki
iliyopita Mahakama ya Kikatiba nchini Uganda ilifutilia mbali sheria
dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, ambayo ilisababisha mataifa kadhaa ya
magharibi kuinyima misaada.
Sheria hiyo ilizua mjadala si tu nchini Uganda bali kote duniani kiasi
cha kuyafanya mataifa ya magharibi yalazimike kuingilia kati.
Mahakama ilisema muswada uliopitishwa kabla ya kuidhinishwa na rais kuwa
sheria, ulipitishwa na wabunge ambao idadi yao haikutosha kuupitisha na
kwa hivyo ulikuwa kinyume na sheria.
Sheria hiyo iliharamisha hatua zozote za kueneza au kushawishi mapenzi
ya jinsia moja na wakati huo huo ikiwajumuisha wanawake wasagaji katika
kundi hilo.
Wabunge nchini Uganda huenda wakalirudisha upya bungeni suala hilo,
mchakato unaotarajia kuwa mrefu ukizingatia sheria ya sasa ilichukua
miaka minne hadi kupitishwa.