Amesema kuwa urais ni taasisi kubwa nchini, hivyo yeye akiwa rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo baadhi ya watu wanaomsukuma ashiriki katika maneno hayo aliyoyaita kuwa ni ya “mitaani.”
“This is nonsense ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” alisema Rais Kikwete alipozungumza na Watanzania wanaoishi nchini Marekani, kwenye Hoteli ya Marriot Washington, jijini Washington D.C, Jumamosi wiki ilitopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa nchini humo, alisema hayo wakati akijibu maswali aliyoulizwa kuhusu madai yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, yaliyompeleka mahakamani.
“Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu, ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu, ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”
Akijibu swali lingine kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, alisema: “Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani.
“Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”
SOURCE: NIPASHE