Serikali ya Uingereza imetangaza mpango wa kujenga kiwanda cha kuzalisha umeme kwa upepo baharini ambacho kitakuwa kikubwa zaidi duniani.
Kiwanda hiki chenye ukubwa wa kilomita 1,725 za mraba kitajengwa kilomita 89 baharini kutoka ufukwe wa mkoa wa York. Kitakuwa na mitambo 300 ya kuzalisha umeme kwa upepo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1,800, na kukidhi mahitaji ya familia milioni 1.8. Mradi huo utajengwa na kampuni moja ya Denmark.
Waziri wa biashara wa Uingereza alisema katika miaka kadhaa iliyopita shughuli za kuzalisha umeme kwa upepo baharini zimepata maendeleo mazuri, na Uingereza inajitahidi kujenga mfumo wa nishati safi wenye usalama.
Serikali ya Uingereza pia inasema hivi karibuni itatenga pauni milioni 730 kuunga mkono miradi ya kuzalisha umeme kwa nishati inayoweza kuzalishwa tena. Inakadiriwa kuwa hatua hii itainua uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo baharini nchini humo kufikia gigawati 10 ifikapo mwaka 2020, na uwezo huo utaendelea kuinuliwa kufuatia kupungua kwa gharama ya uzalishaji.
Mchambuzi wa kikundi cha habari za nishati na hali ya hewa Bw. Jonathan Mashall alisema gharama ya kuzalisha umeme kwa upepo baharini imepungua kwa kiasi kukubwa, na shughuli hii kimsingi inaweza kushindana na uzalishaji wa umeme kwa makaa ya mawe.
Chanzo: inhabitat.com