Afrika ni moja kati ya mabara yaliyosahauliwa katika nyanja ya
teknolojia. Kwa sasa hali hii inaonekana kubadilika baada ya kampuni
mbali mbali kuanza au kuwa na malengo ya kupanua huduma na mauzo ya
kiteknolojia Barani humo. Miongoni mwa kampuni ambazo zimeanza
kulikimbilia Bara hili ni pamoja na Google na Microsoft, kampuni mbili
gwiji katika komputa, tablet, simu na mitandao (IT) kwa ujumla.
Mwezi uliopita Mkurugenzi Mtendaji wa Google Bwana Eric Schmidt ambaye
ametembelea miji mbali mbali ya Afrika ikiwa ni pamoja na Nairobi,
Kigali na Lagos ameweka wazi kuwa Google ina nia ya kuwekeza katika
nyanja ya teknolojia Barani Afrika na hasa katika mji wa Nairobi. Kenya
ni moja wapo ya nchi za Afrika alizozitembelea Bwana Schmidt. Bwana
Schmidt ameeleza uono wake kwamba Nairobi ndio huenda ikawa Silicon
Valley ya Afrika.
Bwana Schmidt amependezwa na maendeleo ya kampuni na miradi mbali mbali
midogo midogo ya kiteknolojia jijini Nairobi kama vile M-Pesa, Kopo Kopo
na eLimu mradi ambao unatengeneza kompyuta za tablet kwa ajili ya
watoto wa shule za msingi nchini Kenya.
Nayo Kampuni ya Microsoft ambayo ina ofisi 14 barani Afrika hivi
karibuni imezindua simu rasmi ambayo inalenga soko la Bara la Afrika
Simu hiyo imetengenezwa na Kampuni ya China Huawei ambayo inachupukia
kwa kasi na kuzitikisa kampuni kubwa za simu Duniani na hasa katika soko
la China. Simu hiyo inatumia OS ya Windows Phone 8 inayotengenezwa na
Microsoft. Simu hiyo inajulikana kama Huawei 4 Africa.
Meneja ya Microsoft Barani Africa Bwana Fernando De Souza ameuelezea
mradi mwengine ambao unaendelea nchini Kenya ambao ni mradi wa kusambaza
Televisheni kwa njia Broadband katika sehemu ambazo hazina umeme kuna
ni mradi wenye mafanikio ambapo Microsoft kwa sasa umewafikishia watu
zaidi ya 6,000 huduma hiyo, pia mipango inaendelea ya kupanua huduma hii
sehemu nyingine barani Afrika. Microsoft hutumia mionzi ya jua (solar
power) kama chanzo cha umeme katika sehemu hizo.
Julai mwaka 2011 kampuni ya kutoa huduma ya simu za mkononi nchini India
imeingia katika nchi 16 kati ya nchi 54 ya Bara la Afrika ikiwemo
Tanzania, Mauritius na Senegal katika mkataba wenye thamani ya zaidi ya
Dola za Kimarekani Bilioni moja na nusu.
Takwimu zinaonyesha kwamba Matumizi ya Internet barani Afrika
yameongezeka kwa zaidi ya 1400% kwa mwaka 2012, ambapo Bara hili ndio
limeongozwa kwa ukuaji wa matumizi ya Internet Duniani.
Katika kile kinachoonekana kulijali soko la Afrika kampuni ya Orange
imedhamini mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika lililofikia kilele
tarehe 10/02/2013 ambapo Nigeria imenyakua ubingwa wa mashindano hayo
kwa mara ya tatu. Nayo Samsung ilimtunukia kiungo wa Chelsea John Obi
Mikel Samsung Galaxy Note II katika kile kinachoonekana kama "utangazaji
wa biashara wa kiuvamizi".
Baidu nayo kampuni iliyoimudu Google kutoliteka soko la Search engine
nchini China kwa imetoa Browser maalum kwa ajili ya Afrika na Asia
katika kile kinachoonekana kama kinyang'anyro cha kuliwahi soko la
Afrika kiteknolojia.
Chanzo: IFM