Serikali ya China imetangaza mpango mpya wa kitaifa kuhusu uvumbuzi wa sayansi na teknolojia katika miaka mitano ijayo, na kuweka malengo ya jumla ya eneo hilo katika miaka mitano ijayo. Mpango huo umesema, hadi kufikia mwaka 2020 China itaingia katika kundi la nchi zenye uwezo mkubwa wa uvumbuzi. Aidha, China pia itaendeleza mfumo wa teknolojia unaohakikisha usalama wa taifa na maslahi ya kimkakati.
Mpango huo umetoa mapendekezo yenye vigezo 12. Kati ya vigezo hivyo, mpango huo umebainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2020, China itainua nafasi yake ya uwezo wa uvumbuzi duniani kutoka 18 ya hivi sasa hadi kufikia 15, kuongeza kiwango cha mchango wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kutoka asilimia 55.3 hadi asilimia 60. Naibu waziri wa sayansi na teknolojia wa China Bw. Li Meng amesema,
"Kushika nafasi ya 15 katika orodha ya nchi zenye uwezo wa uvumbuzi duniani kuna maana gani? Ni kuingia katika kundi la nchi zenye uwezo mkubwa wa uvumbuzi zinazotambuliwa dunia nzima. Hivi sasa China bado haijajiingiza katika kundi hilo. Kuinua kiwango cha mchango wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kutoka asilimia 55 hadi 60, kuongeza kiwango cha thamani za ziada za utoaji huduma za ujuzi katika pato la taifa kutoka asilimia 15.6 hadi 20, hivi ni vigezo muhimu vinavyopima kama viwanda vya taifa vimekua katika mnyororo wa thamani au la."
Mpango huo sio tu unatoa mapendekezo kwa watu binafsi na mashirika, bali pia unataka kuongeza nguvu ya kutoa mitaji katika utafiti wa sayansi na teknolojia kwa upande wa taifa na kutoa pendekezo la kuwekeza asilimia 2.5 ya bajeti hadi kufikia mwaka 2020. Mapendekezo hayo yalitolewa kutokana na tathmini ya jumla ya hali ya maendeleo ya teknolojia ya China.
"Tumewashirikisha wanasanyasi zaidi ya elfu 8 kutathmini hali ya teknolojia ya nchi yetu. Kati ya teknolojia 1,350 za sekta 13 muhimu, asilimia 17 ya teknolojia hizo zimeongoza kiwango cha kimataifa, asilimia 13 zimefikia kiwango cha kimataifa, na asilimia 52 zinafuata kiwango cha kimataifa. Sasa mitaji tuliyotoa katika utafiti wa jamii imefikia dola bilioni 200 za kimarekani, ambayo ni nusu ya mitaji iliyotolewa na Marekani, lakini tumepata mafanikio mengi."
Chanzo: Radio china Kimataifa (cri.cn/)