Bitrina Diyamett, ni miongoni mwa wajumbe 10 wa baraza simamizi kutoka nchini Tanzania, Baraza hilo lilitangazwa siku chache zilizo pita na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusimamia maandalizi ya benki itakayoanzishwa kwa ajili ya kuimarisha teknolojia kwenye nchi zenye maendeleo duni, LDCs.
Bi. Diyamett ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika linalohusika na tafisi za sayansi, teknolojia na ubunifu, SIPRO nchini Tanzania na atakuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza hilo litakaloongozwa na Profesa Mohammed Hassan kutoka Sudan.
Jukumu la baraza hilo la usimamizi ni kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika maandalizi ya kuwezesha benki hiyo kuanza kazi na itatunga kanuni na sera za kuwezesha kuanzishwa, sanjari na katiba itakayozingatiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati wa uzinduzi wake.
Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa kutakuwepo na mfuko maalum wa wadhamini utakaoanzishwa ili kusaidia maandalizi ya benki hiyo ya teknolojia itakayozinduliwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfuko huo unapokea michango kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine ikiwemo sekta binafsi na taasisi nyinginezo.
Chanzo: unmultimedia.org