Wizara ya Elimu ilitoa tangazo hilo siku ya Ijumaa na kuagiza shule za msingi na za upili za serikali kufungwa kote nchini, huku ikifahamisha kwamba uamuzi huo hautoathiri taasisi nyingine za taaluma na vyuo vya mafunzo ya walimu.
Serikali iliongezea kusema kwamba wanafunzi wanaojiandaa kwa mtihani wa kitaifa wa KCSE na KCPE ndio watakaoruhusiwa kubakia shuleni kuanzia mwezi Oktoba ili kufunzwa na walimu wachache ambao hawakushiriki kwenye mgomo.
Maelezo zaidi yanaarifu kwamba ratiba za mitihani ya kitaifa ya KCSE na KCPE ya mwaka 2015 itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Walimu zaidi ya 280,000 wakiongozwa na muungano wao walianzisha mgomo baada ya serikali kushindwa kufikia matakwa yao ya nyongeza za mishahara kwa kiwango cha asilimia kati ya 50-60.
Walimu hao waliapa kuendeleza mgomo wao baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufutilia mbali ombi la nyongeza za mishahara kutokana hali duni ya kiuchumi.