SERIKALI imepiga marufuku vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa katika uwanja wa taifa na kusisitiza, utabaki kwa ajili ya michezo pekee.
Aidha, imekanusha taarifa za kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitafanya mkutano wake wa kufungua kampeni katika uwanja wa taifa.
Ufafanuzi huo ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Alisema, hakuna chama chochote kitakachoruhusiwa kutumia uwanja huo kwa shughuli za siasa.
“Naomba niseme kwa sasa serikali haijaruhusu na hatutaruhusu chama chochote cha siasa kufanya shughuli za kisiasa katika uwanja wa Taifa, uwanja huu utabaki kwa ajili ya shughuli za michezo tu,” alisema Mwambene.
Mwambene alikiri kwamba, Chadema waliandika barua Agosti 12, mwaka huu kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba kufanya mkutano wa ufunguzi wa kampeni zao, Agosti 22.
Alisema waliijibu barua kwa kuwaambia kwamba, uwanja huo upo kwa ajili ya shughuli za michezo na kwamba kwa mazingira ya sasa, hawaruhusu mihadhara ya vyama vya siasa kufanyika katika uwanja huo.
“Haturuhusu Uwanja wa Taifa kutumika kwa mihadhara ya kampeni za vyama vya siasa. Uamuzi huu unalenga kuweka uwanja katika mazingira rafiki ya michezo na kuepuka athari zozote zinazoweza kujitokeza kutokana na mihemuko ya kisiasa,” alisema Mwambene.