MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema siku tatu zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika mfumo wa (BVR) kuhakiki taarifa zao kuwa hazitoshi.
Mbowe alitoa rai hiyo juzi wakati alipokuwa akimtambulisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni feki ya Richmond, Edward Lowassa, ambaye ni mgombea wa urais kupitia Chadema anayeungwa mkono na umoja wa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba wa Wananchi (Ukawa).
Utambulisho huo uliohudhuriwa pia na mgombea mwenza wake, Juma Duni jijiini Mbeya, ulifanyika mbele ya umati mkubwa uliofurika katika viwanja vya Ruanda – Nzovwe, Mbeya pamoja na wenyeviti wa vyama vinavyowakilisha Ukawa akiwemo James Mbatia (NCCR–Mageuzi), Emmanuel Mwakaidi (NLD) na Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima.
Mapema maofisa wa Chadema walionekana katika viwanja vya Ruanda –Nzovwe, wakisajili watu waliohudhuria kwenye karatasi zilizoandikwa; “Kampeni ya watu milioni 15 kwa Lowassa.”
Gazeti hili lilishuhudia maofisa hao waandikishaji wakitoa maelekezo kwa watu waliokuwa wakisajili kuwa taarifa wanazokusanya zitatumika wakati wote wa kampeni kwa kutuma shughuli za kila siku anazozifanya mgombea huyo wa urais kupitia simu ya mkononi. Watu waliojitokeza kwenye kampeni hiyo inayoendeshwa chini chini waliandikishwa majina yao, nambari za simu na wilaya wanakotoka.
“Kampeni za kutumia simu kuwanadi wagombea ni za kawaida katika mataifa yaliyoendelea kama Marekani,” alisema mmoja wa maofisa waandikishaji ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la James.