Ni vigumu kujua mazingira yaliyosababisha kuwapo kwa hali hiyo ya kusikitisha, lakini moja ya sababu zinazotajwa na wataalamu wa masuala ya biashara ni kwamba mamlaka husika zimekosa ubunifu, hivyo zinafanya shughuli hizo kwa mazoea tu. Tatizo ni kwamba zimeweka msisitizo kwenye takwimu zinazoonyesha kwamba mashirika na makampuni yanayoshiriki kwenye maonyesho hayo yanaongezeka, pasipo kufanya tathmini jadidi kuhusu kuongezeka au kushuka kwa viwango na ubora wa ushiriki huo.
Ni kweli kwamba maonyesho ya mwaka huu yamedorora kwa sababu nyingi za msingi. Bunge la Bajeti linaendelea mjini Dodoma, ambapo wabunge, watumishi wa Serikali na taasisi zake wameelekeza vipaumbele vyao kwenye shughuli za Bunge. Pia mwaka huu ni wa uchaguzi na ndiyo maana tunashuhudia jinsi wanasiasa na wafuasi wao kote nchini wanavyozunguka kila kona ya nchi kusaka watu wa kuwaunga mkono, wakiwamo wanaotaka kugombea urais, ubunge na udiwani.
Maonyesho hayo pia yameangukia katika mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambapo ni vigumu kwa waumini wengi wa
Kiislam waliofunga kushiriki katika maonyesho hayo kutokana na
kuingiliana kwa shughuli hizo.
Pamoja na hayo yote, bado tunadhani mamlaka
zinazohusika na maonyesho hayo hazijafanya juhudi za kutosha, kwani
zimeshindwa kutambua kwamba maonyesho hayo yanahitaji matayarisho na
uhamasishaji mkubwa. Matokeo ya kutotambua hilo ni ukimya kutanda kila
mahali kama vile tukio hilo muhimu la kimataifa halifanyiki hapa nchini.
Vyombo vingi vya habari viko kimya kuhusu nini hasa kinaendelea katika
maonyesho hayo na inashangaza kuona mamlaka husika hazijashtukia hali
hiyo. Tovuti husika hazina maelezo ya msingi kuhusu maonyesho hayo,
ambayo baadhi ya watu wameyapa jina la ‘gulio la mwaka’.
Mamlaka husika zinapaswa kutambua kwamba kadri
miaka inavyopita zinapaswa kubadili mbinu, mifumo na mikakati ya
kuendesha maonyesho hayo, kwani mazingira na mahitaji yaliyokuwapo
zamani sasa yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Huko mwanzo nchi yetu
haikuwa na bidhaa muhimu, hivyo wananchi walikuwa wakisubiri maonyesho
hayo kwa hamu kubwa ili wanunue bidhaa adimu, ikiwa pamoja na sabuni,
mafuta ya kupikia na kadhalika. Wengine walisubiri maonyesho hayo ili
kunywa bia kwa sababu kulikuwapo na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo.
Sasa bidhaa hizo na nyingine zipo kwa wingi.
Zinahitajika mbinu mpya za kuwavutia wananchi. Mbinu hizo zilenge
kufungua fursa za kibiashara kama kutafuta wabia na wawekezaji wa ndani
na nje. Maonyesho hayo yalete bidhaa za viwango vya kimataifa ili
wazalishaji wa ndani waige namna ya kuvifikia, lakini katika kufanya
hivyo lazima kwanza mahitaji ya soko yazingatiwe. Ni matumaini yetu
kwamba maonyesho ya mwaka ujao yatakuwa tofauti na miaka iliyopita siyo
tu kwa kuwahamasisha na kuwashirikisha wananchi wengi, bali pia
kuonyesha bidhaa zilizosheheni ubunifu na vipaji.