RAIS Jakaya Kikwete ameidhinisha malipo ya shilingi milioni 230 kwa kila mbunge kama mafao ya kustaafu, Raia Mwema limedokezwa.
Kiasi hicho cha fedha ni sawa na madawati 1916 kwa bei ya shilingi 120, 000 kwa dawati moja na kinaweza kujenga nyumba tano za walimu lakini mbunge atapata kwa kufanya kazi miaka mitano tu.
Awali, ilidhaniwa kwamba Kikwete atapinga malipo hayo makubwa ya kustaafu kwa wabunge katika historia ya Tanzania, lakini gazeti hili limeelezwa kwamba Rais amekubali ongezeko hilo la malipo.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa juu wa Bunge aliliambia gazeti hili mjini Dodoma wiki hii kwamba Rais ameridhia malipo hayo ya mafao yenye kuvunja rekodi na kuwa wapo wabunge ambao tayari wameanza kujichukulia malipo hayo.
“Unauliza kama Rais amekubali mapendekezo ya kuongeza mafao? Mbona Rais ameshakubali na hivi ninavyozungumza nawe wapo wabunge ambao tayari wameanza kuchukua mafao yao?”, alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa maelezo kuwa yeye si msemaji wa taasisi hiyo.
Tume ya Huduma za Bunge ilikuwa imepeleka mapendekezo kwa Rais Kikwete kuomba ongezeko hilo la mafao ya kustaafu kati ya asilimia 75 hadi 85 ambapo jumla ya malipo yote ingekuwa kati ya shilingi bilioni 81.4 na shilingi bilioni 85.
Wakati wa Bunge la Tisa lililokuwa likiongozwa na Spika Samuel Sitta, wabunge waliokuwepo walilipwa mafao ya shilingi milioni 72 kila mmoja wakati waliostaafu Bunge la Nane lililoongozwa na Pius Msekwa walilipwa mafao ya shilingi milioni 20 kila mmoja.
Malipo hayo ya kustaafu yanajumuisha kiinua mgongo (Gratuity) ambayo ni asilimia 40 ya malipo ya mshahara ya mbunge katika jumla ya kipindi alichotumikia bungeni, posho ya hitimisho la kazi (winding up allowance) ambayo ni asilimia 40 ya kiinua mgongo), posho ya usumbufu (relocation allowance) ambayo pia ni asilimia 40 ya kiinua mgongo na posho ya mpito (transitional allowance) ambayo ni mishahara ya mbunge ya miezi mitatu na mafao ya watumishi wa mbunge.
Mashindano ya matanuzi kati ya Bunge na Serikali?
Raia Mwema limeambiwa kwamba awali Kikwete alikuwa akisita kukubaliana na mapendekezo ya Tume hiyo ya Bunge lakini “amekubali kwa sababu hataki kugombana na taasisi hiyo katika mwaka wake wa mwisho wa uongozi lakini pia inaelezwa kuwa wabunge pia wamedai Ikulu pia ina matumizi makubwa kuliko mafao watakayopewa.
“ Kuna mfano ambao umekuwa ukitolewa na wabunge kwa Rais mara kwa mara. Kwamba mwaka uliopita wa fedha, Rais alitengewa kiasi cha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya safari za nje ya nchi lakini ndani ya miezi sita ya bajeti yake alikuwa ametumia mara tatu ya kiasi hicho.
“Swali ambalo wabunge walimuuliza Rais ni kwamba, iweje yeye atumie shilingi bilioni 150 kwa miezi sita kwa safari za nje ya nchi na aone wabunge wote kulipwa shilingi bilioni 82 kama mafao ni tatizo? Nafikiri ndiyo maana Rais aliamua kubadili mawazo,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mfano, Raia Mwema limeambiwa kwamba asilimia 70 ya wabunge wamesafiri mwaka huu kwenda katika miji ya nchi mbalimbali kwa ajili ya ziara za mafunzo; ilhali muda wa Bunge unaelekea ukingoni.
Wakati tunaelekea mitamboni juzi Jumatatu, gazeti hili liliambiwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndiyo kwanza walikuwa wamerejea kutoka katika “ziara ya mafunzo nchini Uganda”.
Baadhi ya kamati na ziara za kikazi walizozifanya mwaka huu pekee kwa ajili ya mafunzo ni Kamati ya Ardhi, Nyumba na Mazingira ambayo ilikwenda Dubai kwa ajili ya mafunzo ya masuala ya mipango miji.
Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo ni Zakhia Meghji na William Lukuvi (kabla hajawa waziri) ambao wamekuwa katika uongozi kwa muda mrefu na ni vigumu kusema walikuwa na lolote la kujifunza kwenye eneo la mipango miji.
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ilitembelea katika miji ya New York, Geneva na Paris kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya serikali iliyoko huko, huku Kamati ya Bunge ya Ukimwi ikitembelea katika nchi za Uganda, Kenya, Zimbabwe na Botswana kati ya Aprili 27 na Mei 04 mwaka huu kwa sababu hizohizo za kujifunza kuhusu mambo ya Ukimwi.
Katika mwaka huuhuu, Raia Mwema limeambiwa kuwa kamati nyingine zimetembelea katika nchi za Singapore, Zambia, Afrika Kusini, Marekani na Malaysia.
“Hebu fikiria, mbunge anaenda kujifunza nini nje ya nchi hivi sasa? Kama capacity building haikufanyika wakati mtu anaanza ubunge, kwenye hili Bunge la mwisho mtu anaenda kujifunza nini? Kuna nini kuhusu Ukimwi ambacho kamati inaenda kujifunza Mei? Tena Uganda?” kilisema chanzo hicho.
Kwa kawaida, mbunge hulipwa kiasi cha kati ya dola 200 -420 (shilingi 400,000 hadi 840,000) kutegemea na nchi anayokwenda wakati anaposafiri nje ya nchi.
Wabunge pia husafiri kwa kutumia tiketi za daraja la kwanza (business class) isipokuwa kama wamepata mwaliko wa taasisi ambayo masharti yake ni kusafiri kwa daraja la kawaida (economy class).
Kwa kawaida, safari za kamati za Bunge huchukua muda wa kati ya wiki moja hadi mbili na ni kawaida kwa wabunge kupata hadi shilingi milioni kumi kwa safari moja kwenye nchi za mbali.
Katika toleo lake namba 369 la Mei 6, mwaka huu, gazeti la Raia Tanzania, ambalo ni gazeti dada la hili liliripoti habari iliyohusu mafao ya kustaafu ya wabunge ambapo wabunge walipendekeza walipwe shilingi milioni 230 kila mmoja, ambalo ni ongezeko la asilimia 75.
Habari hiyo ilieleza; “Uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeandaa waraka na kuuwasilisha Hazina (Wizara ya Fedha) na kwa Rais Jakaya Kikwete, ukiomba kuboresha mafao ya kustaafu ya wabunge kwa asilimia kati ya 75 na 85.
Miongoni mwa sababu za kutaka ongezeko hilo zinazotajwa katika waraka huo uliodokezwa kwa Raia Tanzania ni muda wa ulipaji mikopo ya wabunge.
Kwamba Bunge la Jamhuri litavunjwa mapema zaidi, mwezi Julai, badala ya Agosti, na kwa hiyo, wabunge watalazimika kulipa mikopo yao kwa miezi 57 badala ya 60 hivyo wafidiwe.
Kwa mujibu wa mchanganuo wa malipo uliopelekwa kwa Kikwete, wabunge watalipwa shilingi milioni 31.3 kama posho ya mpito ambapo kwa wote serikali italipa jumla ya shilingi bilioni 11.14.
Mchanganuo kwa nyongeza ya asilimia 75
Katika mchanganuo huo wa malipo ya shilingi milioni 230, malipo ya kustaafu yatakuwa kama ifuatavyo, kiinua mgongo – kila mbunge atapata shilingi milioni 89,4 na kwa hiyo, wabunge wote watalipwa jumla ya mafao ya aina hii shilingi bilioni 31.7.
Kwenye posho ya hitimisho la kazi, kila mbunge atalipwa shilingi milioni 67 na katika aina hii ya mafao, serikali itatakiwa kuwalipa wabunge wote jumla ya shilingi bilioni 23.8.
Pia, kila mbunge atalipwa shilingi milioni 35.75 kama posho ya usumbufu ambayo tafsiri yake ni kwamba serikali itawalipa wabunge wote jumla ya shilingi bilioni 12.7.
Katika posho ya mpito, kila mbunge atalipwa shilingi milioni 11.7 ambapo maana yake ni kuwa jumla ya fedha kwa wabunge wote ni shilingi bilioni nne.
Wabunge pia watalipwa shilingi milioni 25 kila mmoja kama mafao ya watumishi na kwa ujumla wao serikali italipa shilingi bilioni 9.03.
Chanzo: Gazeti la RaiaMwema