
Taarifa makini zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa mabosi wa ngazi ya juu Azam, zimebainisha mpango huo wa kuwataka wachezaji hao raia wa DR Congo walio kwenye kikosi cha kwanza cha Mazembe ambao mmojawao anamudu nafasi ya beki wa kulia na mwingine ni straika.
Chanzo hicho kimefafanua kuwa imekuwa ngumu kuwashawishi wachezaji hao na sasa wamemua kumtumia mshambuliaji wa timu hiyo, Mtanzania, Mbwana Samatta ambaye alikubali na ameonyesha kupata mafanikio makubwa katika kukamilisha zoezi hilo.
Taarifa zinaeleza kwamba awali wachezaji hao ambao mpaka sasa majina yao bado ni siri, walikuwa wagumu walipoelezwa suala la kuhama Congo na kuja kukipiga Tanzania lakini baadaye baada ya kushirikishwa Samatta ambaye ni straika tegemeo wa timu hiyo, sasa mambo yameanza kulainika na mchakato unakwenda vizuri.
“Kuna wachezaji kwa sasa tunawatafuta kwa ajili ya kuweka mambo sawa msimu ujao na kuzidi kusonga mbele zaidi ya hapa tulipo sasa, tayari kuna harakati za kumpata beki mmoja wa kulia na mwingine ni straika, wote raia wa Congo.
“Wanacheza TP Mazembe, tuliamua kumtumia Samatta kwa kuwa awali ilikuwa ngumu kuwapata,” alisema bosi mmoja wa Azam.Gazeti hili lilipomuuliza Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, juu ya suala hilo alikana na kusema:“Hakuna suala kama hilo.”