Mkosoaji mkuu wa serikali ya rais
Yoweri Museveni wa Uganda kupitia mtandao wa kijamii anatarajiwa
kufikishwa mahakamani hapo kesho.
Robert Shaka anakabiliwa na kosa la kutumia mtandao wake wa kijamii wa facebook kinyume na sheria ya matumizi ya kompyuta .Mwandishi wa BBC aliyeko huko Siraj Kalyango anaripoti kuwa bwana Shaka atafikishwa mahamakani kuhusiana na kesi ambayo anadaiwa kusambaza taarifa mbalimbali nyeti kwa usalama wa taifa.
Katika karatasi za mashtaka zilizowasilishwa mahakamani inadaiwa kuwa kati ya mwaka wa 2011 na 2015 akiwa mjini Kampala amekuwa akiingilia maisha ya rais kwa kuchapisha , katika ukurasa wake, hali ya afya ya rais.
Ikulu ya rais Museveni imetoa taarifa ikionya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Sehemu ya taarifa hiyo ya ikulu ya rais inaendelea kusema kuwa vyombo vya dola vilimpelekea rais Museveni barua inayodaiwa kuwa ndiye aliyemuandikia marehemu rais wa Libya kanali Maummar Ghadhafi akikashifu baadhi ya makabila ya kanda ya maziwa makuu.
Rais amekanusha kuandika barua hiyo.
''Mungu amenipa maisha mazuri hata katika umri wa miaka 70 licha ya kupata magonjwa madogo kama vile malaria, na kukohoa kila mara''.
''Kwa hakika hakuna kazi yoyote ambayo siwezi kufanya siku hizi isipokuwa kuchutama ambako kunanipa shida siku hizi''.
Taarifa hiyo ilimnukuu rais Museveni
Hatua hii imekuja baada ya mataifa ya muungano wa ushoroba wa kaskazini kukubaliana kusaidiana kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Mkosoaji mkuu wa serikali nchini Uganda Robert Shaka, alikamatwa jumatano na kufikishwa mahakamani siku iliyofuatia.
Alifungwa rumande katika gereza la Luzira akisubiri kuomba kusikizwa kwa ombi lake la kutaka achiliwe kwa dhamana .
Sheria kuhusu matumizi mabaya ya kompyuta ilipitishwa nchini uganda na kuidhinishwa kuwa sheria mwaka wa 2011.
Wapinzani wa rais Museveni wanasema kuwa sheria hiyo inalenga kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini humo.