Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) Maynard Swai, ametangaza kuwania ubunge katika Jimbo la Hai kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa tangazo hilo, Swai sasa atakuwa na kibarua
kizito cha kukabili upinzani kutoka kwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo,
Freeman Mbowe (Chadema) ambaye tayari ametangaza nia ya kutetea nafasi
yake katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, wakati kurudi kwa Mbowe kwenye
kinyang’anyiro cha ubunge jimboni humo kutategemea uamuzi wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao utalazimika kumkubali au kumkataa
kupitia vikao vyake vya kupanga wagombea. Swai anatakiwa kupita kwenye
kura ya maoni ndani ya CCM, kabla hajawa mgombea rasmi.
Swai ambaye ni kada wa kwanza wa CCM kufungua
pazia la kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Hai, alisema
jana kuwa dhamira yake ni kufanya kazi na wananchi ndani ya jimbo hilo,
tofauti na sasa ambapo wawakilishi wengi wanaomba kura na wakipata
wanahamia Dar es Salam.
“Nimeamua kuingia kwenye siasa niendelee
kuwatumikia wananchi. Ifike mahali kiongozi anayechaguliwa aishi na
wananchi ili ajue shida zao, matatizo yao na changamoto walizonazo na
siyo unapewa heshima na wananchi, lakini ukipata huonekani
ukiwatumiakia,” alisema Swai.
Alisema iwapo chama kitampa ridhaa ya kugombea,
atahakikisha anawaweka vijana pamoja na kutatua changamoto
zinazowakabili likiwemo suala la ajira.