Serikali imeendelea na mikakati ya kuwadhibiti viongozi wa umma wanaokiuka maadili na kushiriki kwenye vitendo vya wizi na ufisadi, ambapo sasa imeunda mwongozo mpya utakaotumika kuwabana.
Mwongozo huo
ambao unatajwa kuwa suluhisho na mwarobaini wa watumishi wezi na
wanaokwenda kinyume, pia utaipa meno zaidi ya kiutendaji, Sekretari ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa sasa sheria
na kanuni zinazoongoza maadili ya viongozi wa umma, lakini kutokana na
sababu mbalimbali, ikiwemo makusudi ama kusahau, baadhi ya viongozi
wamekuwa wakizipuuza, hivyo kusababisha matatizo ya kimaadili, hususan
kuibuka kwa vitendo vya kifisadi.
Kwa mujibu wa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni Mstaafu, George
Mkuchika, mwongozo huo uko katika hatua za mwisho za maandalizi na
utaanza kutumika kwenye mwaka wa fedha 2015/2016.
Mwongozo huo
utaanza kutumia rasmi kabla ya kufanyika kwa matukio makubwa nchini,
ikiwemo kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, ambao
vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili vimekuwa vikishamiri.
Akizungumza
kwenye warsha ya wadau ya kujadili rasimu ya mwongozo huo, Dar es
Salaam, jana, Kapteni Mkuchika, alisema serikali ina nia madhubuti ya
kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili.
Alisema kupitia
mwongozo huo, jitihada za serikali kwenye dira ya maendeleo ya mwaka
2025, zinazosisitiza uongozi bora na utawala wa sheria, zinapewa nguvu
kutokana na uwepo wa programu maalumu zinazohamasisha maadili katika
kila idara ndani ya sekta za umma na binafsi.
Mkuchika
alisema mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaoota mizizi kote
nchini, yanahitaji ushirikiano wa sekta zote, wananchi na asasi za
kiraia, ambapo adui mkubwa kati ya wengi ni rushwa na ufisadi, ambao
kwa kiasi kikubwa unatekelezwa na viongozi wa umma.
Alisema maadili
ya viongozi wa umma ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye
nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kukuza heshima ya
taifa, hivyo serikali inafanya kila linalowezekana kutoa uwezo kwa
Sekretarieti ya Maadili na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), ili matatizo hayo kutoweka nchini.,
Waziri huyo
alisema nchi ilitikiswa na vitendo vinavyotokana na mmomonyoko wa
maadili ya viongozi wa umma katika kipindi kifupi kilichopita, hali
iliyoliletea aibu taifa na kuilazimu sekretarieti ya maadili kuwahoji
watuhumiwa.
Waziri Mkuchika
alisema ni lazima somo la maadili likaingizwa kwenye mitaala ya elimu
kuanzia shule za msingi mpaka elimu ya juu, ili kukomesha tatizo la
ukosefu wa maadili kwa jamii, kwasababu utaratibu uliokuwa unatumika
awali wa kupeleka vijana wote JKT kuwafundisha maadili kwa nyakati hizi
hauwezekani.
Kwa upande
wake, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Jaji Mstaafu
Salome Kaganda, alisema taasisi yake haitaendekeza vitendo vya uvunjifu
wa maadili kwa kiongozi yeyote wa umma awapo kazini au atakapostaafu.
Alisema tangu
kupatikana Uhuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa
ikichukua hatua mbalimbali za kujenga na kukuza uadilifu kwa viongozi wa
umma na sekta ya umma kwa kutumia sera, sheria, kanuni na miongozo,
ukiwemo unaotarajiwa kutumika hivi karibuni.
Jaji Salome
alisema kutumika kwa mwongozo huo ni mwendelezo wa juhudi hizo za
serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, ambapo wakati huu wa kuelekea uchaguzi, viongozi husahau maadili
na kufanya mambo kwa akili zao.
Alisema
watapambana na kila kiongozi anayepotoka kimaadili kwa kutumia miongozo,
kanuni na sheria, ili Tanzania iwe mahali salama kuishi kwa kuzingatia
haki na usawa.
Aidha, alisema
ili kuipa ‘meno’ sekretarieti ya maadili, serikali itaona namna ya
kufanya kuiruhusu imshitaki mtuhumiwa moja kwa moja mahakamani,
wakiwemo wa ufisadi, badala ya kusubiri ruhusa kutoka kwa Mwendesha
Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP).
Sambamba na
hilo, Mkuchika alisema Sekretari hiyo ambayo awali ilikuwa ni kitengo
kidogo cha maadili ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
itapewa hadhi ya kuwa Tume, ili ijitegemee kama ilivyo kwa TAKUKURU.
“Taasisi hii ni
muhimu sana, awali ilikuwa kitengo tu ndani ya jeshi; tukaona umuhimu
wake tukakimegua ,ikawa na hadhi hii, sasa tumeona umuhimu wake zaidi
kwa maendeleo ya maadili ya viongozi nchini, hivyo inabidi iwe tume,
kama ilivyo TAKUKURU,” alisema Mkuchika.