Muswada wa Mahakama ya Kadhi umeondolewa bungeni na sasa hautajadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge unaohitimishwa leo mjini Dodoma.
Huu
ni muswada wa tatu kuondolewa Bungeni baada ya ile miwili ya sekta ya
habari ambayo ni muswada wa Sheria ya kupata Taarifa wa mwaka 2015 na
ule wa sheria ya huduma wa Vyombo vya Habari iliyoondelewa mwishoni mwa
wiki iliyopita.
Muswada huo ulipangwa kuwasilishwa Bungeni leo, lakini serikali imeamua kuuondoa kutokana na hofu ya kutokea mpasuko nchini.
Katibu
wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, akizungumza na mwandishi wetu jana
ofisini kwake alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautakuwapo tena
katika mkutano huo.
Dk.
Kashilila alisema haijulikani ni lini utawasilishwa bungeni kwa sababu
Mkutano wa Bunge ujao unaotarajia kufanyika Mei, utakuwa mahsusi kwa
ajili ya bajeti.
“Waziri
Mkuu alivyosema wataangalia na kushauriana kimsingi, alitoa maneno ya
busara tu au ilikuwa kauli ya mtu mzima, lakini huu muswada
hautakuwapo,” alisema.
Dk.
Kashilila alisema hali iliyojitokeza Jumapili iliyopita wakati wa
semina ya wabunge haikuwa nzuri kutokana na mvutano mkali miongoni mwa
wabunge.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipoulizwa kuhusu kama muswada huo
utawasilishwa bungeni, alisema hakuwa na majibu badala yake alitaka
suala hilo iulizwe ofisi ya Spika.
“Suala hili usiniulize, nenda Ofisi ya Spika au muulize huyu (Magati) ambaye yupo sekretarieti,” alisema huku akiwa na haraka kuelekea ofisini kwake.
Naibu
Spika, Job Ndugai, akizungumza na mwandishi nje ya ukumbi wa Bunge
muda mfupi baada ya kuahirisha Bunge, alisema muswada wa Mahakama ya
Kadhi hautawasilishwa bungeni leo.
“Huo muswada hauwezi kuletwa bungeni kutokana na hali ilivyo,” alisema Ndugai bila kufafanua zaidi.
Naye
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro, alipoulizwa kama
muswada huo utawasilishwa bungeni alimtaka mwandishi asimuulize maswali
yanayohusiana na muswada wa Mahakama ya Kadhi.
“Sitaki kabisa kuulizwa suala la Muswada wa Mahakama ya Kadhi, “alijibu Dk. Migiro kwa hasira huku akiingia kantini.
Tujikumbushe
Februari
mwaka huu, muswada huo pia uliondolewa bungeni kwa kile Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alichodai kwamba ni kwenda kuonana na viongozi wa dini
kuwaelemisha juu ya mahakama hiyo, ili uwasilishwe tena kwenye mkutano
unamalizika leo.
Mwishoni mwa wiki nusura wabunge wazipige kavu kavu huku wakirushiana maneno wakati wa semina kuhusu Mahakama ya Kadhi.
Kutokana
na joto lilivyopanda, baadhi waliamua kususia semina hiyo na kutoka
huku wengine wakibaki na kurushiana vijembe. Semina hiyo iliandaliwa na
Bunge.