Walinzi wa hospitali hiyo walimuokoa mrembo huyo kwa kumnasua mikononi mwa wagonjwa hasa wajawazito walioenda kujifungua, waliodai kwamba Mariam aliingia katika wodi yao na kuwaibia.Tukio hilo lilitokea Machi 27, mwaka huu saa tisa alasiri, ambapo mama mmoja ndiye alishtuka kwa kuona amechukuliwa kitenge chake kipya.
Mama huyo alipobaini ameibiwa, alitoka nje na kuangaza macho huku na kule akiangalia alipoelekea Mariam aliyekuwa wodini kwao, ndipo alipomuona akiwa anatoka nje kulielekea geti ambapo aliwapigia kelele walinzi ili wamzuie.
Hata hivyo, walinzi walipompekua, aligundulika kuwa na vitu alivyovifunga na kufunika kwa dera (gauni kubwa, refu alilokuwa amevaa).Askari wa kike walipomfunua gauni hilo, walimkuta akiwa na taulo ambalo alikuwa amelifunga kiunoni pamoja na kitenge alichokuwa akituhumiwa kukiiba wodini.
Baada ya wagonjwa kuona mali alizoiba mrembo huyo, ndipo akina mama wengine wakiwa na watoto wao walitoka wodini na kuanza kupiga makelele kwa hasira wakitaka apewe mkong’oto.
Aliomba msamaha kwa kitendo alichokifanya, akisema kinatokana na maisha magumu na katika hali ya kushangaza zaidi, alipoulizwa kuhusu taulo alilokuwa amejifunga ndani ya dera alilovaa, alisema halikuwa la hospitalini hapo, bali aliliiba katika gesti aliyokuwa amelala siku hiyo.
CHANZO: GPL