Bado hakuna mwafaka kuhusu hatima ya Katiba Mpya, baada ya kuahirishwa kwa upigaji Kura ya Maoni iliyopaswa ifanyike Aprili 30 mwaka huu.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na baadhi
ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisema Kura ya Maoni itafanyika
wakati wowote mwaka huu baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura kwa
Mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR), wanaharakati na viongozi
wa vyama vya upinzani, wanaamini kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni,
kungetoa fursa ya mchakato huo kurudi kwenye Bunge la Katiba.
Wapinzani hao wanasema hili litasaidia kuondoa
tofauti zilizojitokeza wakati wa Bunge la Katiba ambako kundi hilo
lilisusa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, wapo wanaoamini pia kuwa kuahirishwa
kwa Kura ya Maoni, ndiyo mwisho wa Mchakato wa Katiba Mpya, hasa baada
ya rais aliyeanzisha mchakato huo kumaliza muda wake baada ya uchaguzi
mkuu.
Nec iliahirisha Kura ya Maoni iliyopaswa kufanyika
Aprili 30 mwaka huu kutokana na kulegalega kwa shughuli ya kuandikisha
wapigakura kwa BVR na baada ya tamko hilo giza likagubika hatima ya
mchakato mzima.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na
mabadiliko yake yaliyofanyika mwaka 2012 na Sheria ya Kura ya Maoni ya
mwaka 2013, ziko kimya juu ya nini kinafuata baada ya kuahirishwa kwa
Kura ya Maoni.
Sheria hizo zimeeleza tu namna Mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba unavyopaswa kuendeshwa kuanzia siku ulipotangazwa
hadi kupatikana kwa Katiba Mpya. Pia sheria zimeeleza nini kitafuata
kama kura ya NDIYO haitafika zaidi ya 50 kutoka pande zote za Muungano.
Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Kura ya Maoni na
Kifungu cha 36(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinasema kama kura
za ndiyo hazifiki zaidi ya nusu ya wapigakura wote Bara na Zanzibar,
Tume ya Uchaguzi Nec, na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa makubaliano
maalumu na baada ya tangazo la Serikali, watachagua njia nyingine ndani
ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo hayo.
Ikifikia hapo mchakato wa upigaji Kura ya Maoni
utaanza upya. Sheria zote zimempa Rais mamlaka ya kuitisha tena Bunge la
Katiba kubadili vipengele vilivyokataliwa wakati wa upigaji kura.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria ya Kura ya Maoni
pamoa ja na Kifungu cha 36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
vinasema, kama kura za HAPANA zitakuwa nyingi ikilinganishwa na kura ya
NDIYO, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
itaendelea kutumika.
Vyama vya upinzani kupitia Umoja wao wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wamekuwa wakitaka Kura ya Maoni iahirishwe ili kukaa
na kutafuta kwanza mwafaka katika baadhi ya mambo ikiwamo Muundo wa
Muungano.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa Ibrahim Lipumba,
amesema siyo sahihi kuendelea na mchakato wa Kura ya Maoni, kabla ya
kupitia upya maeneo yaliyoleta mpasuko kwenye Mchakato wa Katiba.