WAKAZI wa Ekalakala, eneo la Masinga, Kaunti ya Machakos, mapema wiki hii wakishirikiana na polisi walilifunga kanisa moja eneo hilo kwa madai kuwa waumini wake wanaabudu wakiwa uchi.
Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Masinga,
Bw Muraya Mwangi, alisema amekuwa akipokea malalamishi kutoka kwa umma
kuwa wanawake wanaohudhuria ibada katika kanisa hilo hutakiwa kuvua nguo
wakiombewa.
Bw Mwangi alisema kanisa hilo la Healing Ministry ni la wanawake pekee na kwamba halina ratiba au saa mahususi za ibada.
“Baadhi ya wanawake walipatikana
wakiwa uchi ndani ya kanisa hilo chifu wa eneo hilo alipolivamia
akiandamana na wakazi,” akasema Bw Muraya.
Afisa huyo aliongeza kuwa kasisi wa
kanisa hilo, Joseph Wambua, amekuwa akiongoza kanisa kinyume cha sheria
kwa sababu hana stakabadhi zinazohitajika.
Mwenyekiti wa muungano wa
wafanyabiashara wa kituo cha biashara cha Ekalakala, Bw Duncan Mutua,
alithibitisha hayo na kusema shughuli za kanisa hilo zimekuwa
zikifuatiliwa kwa makini baada ya wakazi kulalamikia kuwa linaendesha
'ibada chafu.’
“Kasisi wa kanisa hilo amepatikana
mara kadha akiwaombea wanawake wakiwa uchi wa mnyama ndani ya kanisa na
hatimaye hatua imechukuliwa,” akasema Bw Mutua.
Aliongeza kuwa wasiwasi kuhusu
shughuli za kanisa hilo uliongezeka baada ya wanawake wa eneo hilo
kutumia muda wao mwingi kanisani na hata kuacha waume wao usiku kwenda
kwa ibada za 'kesha.’
“Tulivamia kanisa hilo na kumfumania
kasisi akiwamwagilia wanawake maji wakiwa uchi wa mnyama. Alijitetea
akisema alikuwa akiwafanyia maombi spesheli,” akasema.
Alisema baadhi ya wanawake ambao ni waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakizozana na wanaume wao tangu kanisa hilo lifungwe.
Kuhubiri injili
Lakini Kasisi Wambua alikanusha
madai hayo na kuyataja kuwa ya uwongo akisema kanisa lake limekuwa
likihubiri injili eneo hilo kwa 'njia zinazofaa’ na kuwalaumu maafisa wa
utawala wa eneo hilo kwa kudai hongo kutoka kwa kanisa hilo kila mwezi.
“Shida hizi zote zimesababishwa na machifu wa eneo hili ambao wamekuwa
wakidai hongo kutoka kwangu,” akasema Bw Wambua.
“Hili ni kanisa linalomcha Mungu na
madai haya yote hayana msingi wowote,” akaongeza. Maafisa wa polisi
walisema kanisa hilo litafungwa hadi uchunguzi kuhusu shughuli zake
ukamilike.
Wakazi wa Masinga wanasema kanisa
hilo lilivutia waumini wengi kutoka kanisa la Africa Inland Church (AIC)
ambalo lina wafuasi wengi kutoka eneo hilo. “Lilianzishwa mwaka
uliopita na baada ya miezi sita lilikuwa limevutia zaidi ya waumini 100
wengi kutoka AIC,” akasema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake
litajwe.
Inasemekana Bw Wambua aliripoti
kufungwa kwa kanisa lake kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Masinga ambaye
aliagiza machifu wafike afisini mwake jana.