Ujasiriamali
ndio neno jipya. Kila mtu anaongelea habari za ujasiriamali. Pengine
hii inatokana na wengi wetu kutambua kwamba nyakati zimebadilika na
ujasiriamali ndio njia iliyo sahihi zaidi kama mtu anatamani mafanikio
ya kweli maishani.Vijana ndio chachu zaidi ya ujasiriamali au naweza
kusema ndio wanategemewa zaidi kuendeleza ujasiriamali hususani katika
ulimwengu wa leo wa sayansi na tekinolojia.
Pamoja na nia nzuri
walizonazo vijana, pengine ukiwemo wewe unayesoma makala hii, kipo
kizingiti ambacho ni lazima watu wajifunze mbinu mpya za kukivuka.
Kizingiti hicho ni aina ya elimu itolewayo mashuleni. Kwa bahati mbaya
elimu zitolewazo mashuleni bado hazijawekwa katika msingi unaomuwezesha
kijana kujiajiri au kwa maneno mengine kuwa mjasiriamali pindi amalizapo
masomo yake.
Bado tupo katika ule
mfumo wa kikoloni. Ukimaliza shule unachotakiwa ni kuanza kutafuta
kazi. Zunguka jijini Dar-es-salaam kwa mfano, utakutana na vijana wengi
wasomi waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini wakiwa wamebeba
vyeti vyao kwenye bahasha wakizurura kusaka ajira. Hakuna anayefiria
kujiajiri kwa kutumia elimu aliyoipata chuoni. Kwanini? Ndivyo ilivyo.
Elimu aliyopewa haikumuandaa.Utakutana na engineer wa umeme ambaye
hajawahi kubadilisha hata balbu!(nimeongeza chumvi kidogo hapa lakini
kuna ukweli ndani yake!) Amesomea nadharia zaidi ya vitendo. Utakutana
na mwanafunzi mhitimu wa masomo ya kilimo na mazingira ambaye hajui
shamba ni nini.Hilo ni kosa katika mfumo wetu wa elimu. Ni lazima
serikali ichukue jukumu la makusudi kubadili mfumo huo.
Lakini wapo wengine
wengi ambao wana nia ya kweli ya kuwa wajasiriamali. Wana nia ya
kujiajiri. Leo tutaangalia jinsi gani mjasiriamali chipukizi aanzishe
kampeni yake. Je ushasikia kwamba biashara siku hizi ni kujuana?
Ujasiriamali pia. Ni muhimu sana kujua ni nani au ni wapi uende endapo
mambo yatakwama. Siongelei wapi uende kutoa au kupokea rushwa.La. Nataka
kuongelea kitu kinachoitwa na wenzetu wa magharibi “networking”.Kwetu
sisi hiki ndicho tunachoita “mtandao”.Mitandao ya kijamii kama vile
facebook,twitter,myspace nk ni sehemu nzuri ya kutengeneza
network.Itumie vizuri.
Ni muhimu
kutengeneza mtandao mzuri kama unataka kuwa mjasiriamali makini na
hususani kama unataka kufanikiwa. Kumbuka kwamba hapa hatuongelei
kubadilishana business cards peke yake baali kumjua mtu kwa nia njema ya
kusaidiana.Kumbuka neno ni “kusaidiana” na sio wewe pekee kupokea
msaada.Lazima pawe na nia njema ya kusaidiana.
Kabla sijaanza
kuorodhesha mbinu mbalimbali za kutengeneza ‘mtandao’ wako, naomba
nikwambie kwamba siri ya kwanza ya kuanza kuwa mjasiriamali ni
maandalizi.Jiandae kwa mtaji,elimu(ya darasani na mtaani),mbinu za
kibiashara nk. Pili hakikisha kwamba una mapenzi ya dhati na hicho
unachotaka kufanya.Usiingie kwenye biashara au ujasiriamali kwa sababu
tu umemuona fulani amefanya hivyo.Kuna umuhimu mkubwa wa kujitambua
katika suala zima la ujasiriamali. Baada ya kusema hivyo,sasa tuingie
kwenye maeneo ya kutengeneza mtandao wako kama mjasiriamali;
- Washindani wako: Biashara ni ushindani lakini sio uadui.Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio ni vizuri sana ukawajua washindani wako wa kibiashara.Pata vipeperushi vyao,tembelea tovuti zao,wajue wateja wao na kwanini hao watu ni wateja wao.Kisha jitambulishe kwao.Najua hapa unasema;nijitambulishe?!! Ndio,jitambulishe.Kama nilivyosema ni washindani lakini sio maadui zako. Mshindani wako anaweza kukufaa pia.Anaweza kuzidiwa na kazi akakusukumia zingine.Jitambulishe,jenga uhusiano mzuri wa kibiashara.Isitoshe nyote mpo kwenye biashara moja,sekta moja.Ya kesho hamyajui.Kama kuna chama au ushirika wa watu waliomo kwenye eneo lako la ujasiriamali,jiunge.
- Vyombo vya Habari: Siku hizi kuna aina nyingi zaidi za vyombo vya habari na mawasiliano. Kuna magazeti,televisheni,radio, blogs nk. Kama mjasiriamali,ni muhimu ukajuana na watu wanaoendesha au hata kumiliki vyombo hivi vya habari. Na zaidi angalia vile ambavyo vipo karibu zaidi na eneo lako la ujasiriamali.Ni rahisi zaidi kwa habari ya ujasiriamali wako kuandikwa gazetini,kuongelewa radioni,kuonekana kwenye televisheni nk kama watu wa vyombo vya habari wanajua unachofanya.Mara nyingi watu wengi wa habari wanapotaka kufanya utafiti wa jambo fulani huanza kwanza kwa kuangalia “sources” alizonazo. Kumbuka kwamba kuandikwa mara kwa mara juu ya kazi zako,ujasiriamali wako, husababisha watu kukukumbuka,kukuheshimu na hivyo kuwa rahisi kwao kufanya biashara na wewe.
- Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO): Mjasiriamali makini ni yule ambaye anadhamiria kuisaidia jamii yake kwa njia moja au nyingine. Zipo faida mbalimbali za kibiashara kwa mjasiriamali ambaye hurudi nyuma na kusaidia jamii yake.Kuna faida za mapunguzo au unafuu fulani wa kodi(waulize TRA watakupa data zaidi).Isitoshe jamii iliyo bora,iwe kiafya,kielimu nk ni wateja wako wazuri wa siku za mbeleni.Hivyo ni muhimu kujuana na watu mbalimbali wanaoendesha mashirika yasiyo ya kiserikali ama NGOs.Dhamini shughuli zao mbalimbali.Ukifanya hivyo(mara nyingi ni bei rahisi zaidi) unakuwa umesaidia jamii yako na pia umetangaza biashara yako.Lakini kuwa makini. Zipo NGO kibao siku hizi.Nyingine ni mitaji ya watu.Achana nazo.Tafuta zile ambazo ni halali na kazi wanayofanya inaonekana katika jamii.
- Mwanasheria mmoja au wawili: Kama ilivyo katika maeneo mengine,msaada wa kisheria unaweza ukahitajika wakati wowote katika ujasiriamali.Unaweza kutaka ushauri,unaweza kushitakiwa nk. Ni vizuri kama ukawa unajuana na watu mbalimbali waliopo kwenye uwanja wa wanasheria. Mara nyingi watu tunaelewa mambo vizuri tunapokuwa tunaongea na watu ambao tunafahamiana nao kwa njia moja au nyingine.Wazungu wanasema unakuwa “more comfortable”. Sasa kwa sababu huwezi jua ni lini utahitaji msaada wa kisheria, ni vizuri ukajuana na mwanasheria mmoja au wawili kwa minajili ya kukusaidia endapo utaalamu wao utahitajika.Kumbuka tu kwamba hapa siongelei msaada wa bure bali malipo fulani ingawa kutokana na kujuana huko,ni rahisi kupata punguzo la bei na pia ile faraja ya kuongea na mtu unayejuana naye.Wakati mwingine unaweza kumuuliza tu “rafiki mwanasheria” kuhusu hoja fulani ya kisheria wakati wa chakula cha mchana(lunch) na ukawa umepata jibu.Free.
- Mwakilishi wako wa kisiasa:
Bahati mbaya au nzuri ni kwamba hakuna biashara au ujasiriamali ambao
unaweza kujitenga moja kwa moja na siasa za nchi au eneo fulani. Kuanzia
kwenye ugawaji wa maeneo ya biashara, utolewaji wa leseni za
biashara,sera mbalimbali za biashara nk lazima kuna ‘siasa’ fulani. Sasa
kwa sababu sera hizo huwa zina mkono wa siasa,ni muhimu sana kujuana na
wahusika au watungaji wa sera hizo ambao mara nyingi ni
wanasiasa.Ukiwajua au kujuana na wanasiasa wa eneo lako,ni rahisi kwako
wewe kufikisha ujumbe,malalamiko yako na pia hisia zako katika mambo
mbalimbali.Kumbuka kwamba biashara au ujasiriamali wako ni sehemu ya
jamii.Ni muhimu ukamjua Balozi,Mjumbe,Mbunge,Waziri nk kutoka katika
jumuiya yako au mahali ilipo biashara yako.Usije kujidanganya kwa kusema
‘ah mimi sitaki kabisa kujuana na wanasiasa”.Utakuwa unakosea na
utakuwa sio mjasiriamali makini.