Vurugu, matusi ya nguoni, kejeli, kelele na zomeazomea vilitawala jana
katika semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Mahakama ya Kadhi,
baadhi wakitaka uwasilishwe bungeni kama ilivyopangwa na wengine
wakitaka uondolewe, hali iliyosababisha baadhi yao kutaka kupigana.
Semina hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala na kufanyika katika ukumbi wa Msekwa, ilianza saa 5.04 asubuhi
hadi saa 10.20 jioni, huku wabunge wakiishushia lawama Serikali, hususan
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutaka kuwasilisha muswada huo bungeni
bila kuwashirikisha, kwa kina, Waislamu na Wakristo.
Katika mvutano huo nusura Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses
Machali ashikane mashati na Mbunge Konde (CUF) Khatib Said Haji na
Mbunge wa Chwaka (CCM) Yahya Kassim Issa baada ya kupishana kauli.
Semina hiyo iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria,
William Ngeleja ilihudhuriwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri
Mkuu Pinda, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro; Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju huku Jaji Dk Robert Makaramba wa
Mahakama Kuu akipewa jukumu la kutoa mada kuhusu Mahakama ya Kadhi.
Hali ya kutoelewana ilianza kuonekana hata kabla ya kuanza kwa semina
hiyo kutokana na wabunge wengi kupanga kukwamisha muswada huo kujadiliwa
bungeni kwa madai kuwa utaleta udini na kuligawa Taifa.
Wabunge waliotoa maneno makali katika semina hiyo ni Mbunge wa Fuoni
(CCM), Said Mussa Zubeir na Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden
Rage.
Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya Mbunge wa Kisarawe (CCM),
Suleiman Jaffo alipokuwa akichangia kuwataka wabunge Waislamu kukutana
baada ya semina hiyo.
“Serikali isifanye masihara juu ya muswada huu. Wanachotakiwa kufanya ni
kukubali ujadiliwe bungeni na huko bungeni ndiyo tufanye marekebisho,”
alisema Jaffo.
Kauli hiyo ilipingwa na Machali ambaye alimwambia anazungumza kitu
ambacho hakijui, kitendo ambacho kilisababisha Yahaya Kassim Issa na
Khatibu Saidi Haji kusimama kwenye viti vyao na kwenda ‘kumtia adabu’,
kabla ya kuzuiwa na wenzao waliokuwa karibu nao.
Vurugu na kelele viliendelea kwa takribani dakika 20 huku baadhi ya
wabunge wakitoka nje ya ukumbi huo licha ya kutakiwa kutofanya hivyo na
Spika Makinda. Kutokana na hali hiyo, Polisi walilazimika kuingia katika
ukumbi huo kwa lengo la kutuliza vurugu.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu alisema Waislamu wanapaswa kulia na Pinda kuhusiana na Mahakama ya Kadhi.
“Waislamu nawaambia kama mtu wa kulia naye ni Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye ndiyo chanzo cha kutopatikana,” alisema