BUNGE wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rosweeter Kasikila (60), amejikuta kwenye kashfa nzito ya kufunga ndoa na kijana, kinda wa miaka 26, Michael Christian.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG), linaloongozwa na Mchungaji Getrude Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, imebaki kuwa gumzo na kuwaacha hoi baadhi ya mawaziri, wabunge wanaoifahamu pamoja na majirani wanaoishi na mbunge huyo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya wanandoa hao na majirani wanaowazunguka, vililiambia gazeti hili kuwa ndoa hiyo ilifungwa Septemba Mosi mwaka 2011, na imebaki kuwa siri kabla ya wawili hao kukorogana.
Kabla ya wawili hao kuamua kufunga ndoa, mbunge huyo kutoka mkoani Rukwa, mwenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, alikuwa akimtumia Michael kwenye shughuli mbalimbali na muda wote alikuwa akiishi nyumbani kwa mbunge huyo.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo ambaye ana familia ya watoto wawili ambao kiumri wanalingana na Michael, alianza uhusiano wa kimapenzi na kijana huyo kwa siri kubwa na baadaye alifanikiwa kumshawishi wafunge ndoa huku akimuahidi kumpa huduma mbalimbali anazotaka.
Kwa mujibu wa habari hizo, wawili hao waliamua kufunga ndoa katika Kanisa la TAG baada ya mbunge huyo kufanikiwa kumshawishi Mchungaji Rwakatare kwamba ndoa hiyo itakuwa siri, hasa kutokana na tofauti ya kiumri kati yao.
Hata hivyo ndoa hiyo kwa sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa, huku mbunge huyo akidaiwa kuzuia kila kitu cha mumewe huyo, hasa vyeti vyake vya shule kama njia ya kumbana warudiane.
Siku ya harusi
Kwa mujibu wa mashuhuda wa harusi hiyo ya aina yake, mbunge na kijana huyo walikwenda kanisani wakiwa wawili bila mashahidi kama ilivyo kawaida, na ndoa hiyo ilifungwa katika ofisi ya kanisa na sio ndani ya kanisa.
Mashahidi wa ndoa hiyo waliitwa hapo hapo kanisani na walisimamia na kushuhudia utiaji saini wa cheti cha ndoa na kisha wanandoa hao kutawanyika kwenda kwenye fungate (Honey Moon). Hakukuwa na sherehe baada ya kufungwa ndoa.
Inadaiwa kuwa hakukuwa na ndugu yeyote wa maharusi hao aliyeshuhudia tukio hilo la kihistoria la wawili hao kuunganishwa na kuwa mwili mmoja.
Kauli ya Bwana harusi
Tanzania Daima Jumatano, lilifanikiwa kumpata Michael, ambaye katika mazungumzo yake alikiri kufunga ndoa na mbunge huyo Septemba Mosi mwaka 2011, lakini kwa sasa wametengana kutokana na sababu ambazo hakutaka kuziweka wazi.
“Mimi nadhani hili ni jambo binafsi, sio vizuri kulizungumza hadharani ila kweli nilifunga naye ndoa maana inaonekana mnajua mambo mengi kunihusu, na ni kweli kwa sasa tumeachana,” alisema kwa kifupi.
Alisema walikutana na mbunge huyo Bagamoyo wakati alipokuwa akifanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali ya wilaya hiyo kama muuguzi mkunga wakati mbunge huyo akiwa muuguzi mkuu wa wilaya katika hospitali hiyo.
Alipoulizwa sababu za kukubali kufunga ndoa na mama wa umri wa miaka 60 wakati ana miaka 26 na sababu za ndoa hiyo kuvunjika, Michael alisema ana historia ndefu katika maisha yake kwani alizaliwa yatima na amekua na kulelewa kwa ufadhili wa kituo cha Safina Street Network.