Ukizisoma Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (Police General Orders) au kwa kifupi PGO, zimetoa mwongozo mzuri wa namna ya kutekeleza majukumu ya kipolisi. Lakini kubwa zaidi ni usimamizi wa nidhamu kwa askari.
Tumeona tuanze kujenga hoja ya rai yetu kwa
kutumia PGO kutokana na mlolongo wa matukio yanayolikumba jeshi hilo,
ikiwamo tukio la juzi katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo mkoani
Iringa.
Ni mwendelezo wa matukio ya kusikitisha ambapo
sasa wananchi wamefikia hatua mbaya ya kuharibu mali za jeshi hilo, kwa
kuchoma moto vituo vya polisi na magari yao.
Uvamizi na uharibifu wa mali za Jeshi la Polisi
unaofanywa na wananchi siyo wa kupongezwa, ni kichaa tu ndiye atawaunga
mkono wananchi hao. Hatuna haja ya kuorodhesha matukio hayo sababu
yanafahamika.
Miaka ya nyuma polisi walikuwa wakiheshimika sana
na siyo hivyo pekee hata woga kwa polisi ulikuwa mkubwa. Kipindi hicho
watu walitii sheria bila shuruti, kwa sababu polisi wenyewe walitii na
kuitekeleza kwa vitendo PGO bila shuruti.
Ripoti nyingi za utafiti zinawataja polisi kwamba
wako nafasi za juu kwa kuomba rushwa, kwa ujumla yanayotokea ni kwa
sababu nidhamu ndani ya Jeshi la Polisi haipo, ndiyo maana wananchi
hawana heshima wala woga kwa polisi.
Siku hizi ni kawaida mtuhumiwa au mhalifu
kubishana na polisi, tena wanapatana hata kiasi cha rushwa. Mengi
yanazungumzwa, askari kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu hadi anazoeana
na wahalifu, kuishi uraiani, lakini kubwa zaidi ni nidhamu.
Siku hizi, askari hawafuati misingi ya upolisi kama ilivyo kwenye PGO. Misingi inasema, kwa mfano, askari hatakiwi kuacha lindo hadi mwenzake afike lakini siku hizi askari anaacha lindo kabla mwenzake hajafika.
Ni jambo la kawaida siku hizi kuona askari
akiingia kazini huku amelewa. Lakini kwenye PGO unaambiwa kabla askari
hajaingia lindoni ni lazima akaguliwe lakini siku hizi hilo halifanyiki.
Wakati wa kumtafuta mrithi wa IGP Said Mwema
gazeti moja lilitabiri maofisa watatu, Thobias Andengenye, Ernest Mangu
na Diwani Athumani. Lakini sifa pekee ya Mangu ilikuwa ni usimamizi
mzuri wa PGO.
Utabiri huo ulikuwa kweli kwa Mangu na baada ya
uteuzi zilitajwa sifa zilizompa alama nyingi kwenye kupata wadhifa wake
huo ikiwamo namna anavyofahamika kwa usimamizi wake wa PGO, hasa
usimamizi wa maadili ya uaskari.
Tungependa kusisitiza kuwa kaulimbiu ya “Nidhamu
ni nguzo thabiti katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi”,
iliyotumika kwenye mkutano wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi
uliofanyika mkoani Dodoma mwezi uliopita iendelezwe kwa vitendo. Bila
polisi wenyewe nidhamu hakuna atakaye waheshimu wala kuwaogopa.