Mahakama
ya Hakimu Mkazi Bukoba mkoani Kagera, imewavua nyadhifa zao madiwani
sita (6) wa manispaa ya Bukoba na kutangaza kuwa kata zao zipo wazi
baada ya kuwatia hatiani kwa kugoma bila sababu kuhudhuria vikao
vilivyoitishwa kwa mujibu wa sheria.
Akisoma hukumu katika shauri lililofunguliwa na diwani wa kata ya Kahoro Mheshimiwa Chief Karumuna, hakimu wa mahakama hiyo mheshimiwa Charles Wisso, amesema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kuwa madiwani hao walivunja sheria kwa kutohudhuria vikao vilivyoitishwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Aidha katika hukumu hiyo mahakama imeamuru madiwani hao kulipa gharama zote za kesi na kuagiza kuwa waziri mwenye dhamana ajulishwe kuwa madiwani sita wamepoteza sifa hivyo kata walizokuwa wakiwakilisha zipo wazi, tangu baada ya hukumu hiyo.
Awali
kabla ya kusoma hukumu hiyo iliyochukua takribani saa moja na nusu,
hakimu Wisso amesema kuwa mlalamikaji aliwatuhumu madiwani hao kwa
kususia vikao kwa maelekezo ya mbunge wa Bukoba Mjini Baalozi Khamis
Kagasheki na hivyo kuiomba mahakama itangaze kuwa madiwani hao walikuwa
wamepoteza sifa.
Hakimu
Wisso pia amesema utetezi wa madiwani hao haukuwa na sababu za msingi
za kutohudhuria vikao na hivyo madiwani sita kutiwa hatiani kati ya
madiwani nane (8) waliolalamikiwa.
Madiwani
waliopoteza viti vyao, ni pamoja na Yusuph Ngaiza wa kata Kashai, Dauda
Karumuna wa kata Ijuganyondo, Deus Mutakyahwa wa kata Nyanga, Samwel
Ruhangisa wa kata Kitendaguro, Murungi Kishwabuta na Rabia Badul ambao ni madiwani wa viti maalum.
Chama Cha Mapinduzi CCM kimepoteza madiwani watano (5) huku Chama Cha Wananchi CUF kikipoteza kiti kimoja.