Hali ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro aliyejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi mbili juzi huko Kibamba, Dar es Salaam inazidi kuimarika na jana alizungumza na Mwananchi na kusema; “Sijambo, naendelea vizuri.”
Ufoo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hata hivyo, anazungumza kwa shida kutokana na kukabiliwa na maumivu baada ya kufanyiwa upasuaji juzi.
Mwandishi huyo amehamishiwa katika wodi ya upasuaji wa moyo huku kiongozi wa wodi hiyo, ambaye alikataa jina lake kuandikwa, akieleza kuwa walimhamishia huko ili apate muda zaidi wa kupumzika.
“Watu wanakuja kwa wingi kumjulia hali, tuliona tumhamishe ili apumzike,” alisema kiongozi huyo.
Kabla ya kupelekwa katika wodi hiyo, Ufoo alikuwa katika wodi ya Kibasila na baadaye alihamishiwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Ufoo alipigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye. Pia Mushi anatuhumiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro wakati wa tukio hilo.
Mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa huko Machame mkoani Kilimanjaro.
Ufoo aongea kwa shida
Mara baada ya mwandishi wa Mwananchi jana kuingia
katika chumba alicholazwa Ufoo huku akisindikizwa
na wauguzi watatu, mwandishi huyo alitoa mkono wake na kusema; “Njoo
hapa unisalimie huku umenishika mkono.”
Huku akionyesha uchovu na kusikia maumivu, alizungumza kwa tabu na kusema; “Sijambo naendelea vizuri.”
Mara baada ya wauguzi hao kumweleza kuwa kati ya waandishi zaidi ya 30 waliofika kumjulia hali ni watatu tu ndiyo walioruhusiwa kumwona alitaka kujua ni kina nani waliobaki nje kwa kuhoji; “Nani hao wako nje.”
Hata hivyo, wauguzi hao hawakutoa nafasi yoyote kwa Ufoo kuulizwa maswali.
Ufoo alipigwa risasi moja tumboni, iliyotokea kwenye mbavu na nyingine ilipita kifuani hadi kwenye ziwa lake la kulia hadi kwenye mkono wa kulia.
Baada ya tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.
Awali Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alifika katika hospitali hiyo kwa lengo la kuzungumza na mwandishi huyo, lakini alizuiwa na kutakiwa kwenda ofisi za utawala ili kupewa kibali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Redio One, Joyce Mhaville alisema kuwa Ufoo anahitaji muda wa kupumzika ili apone.
“Ufoo ana kumbukumbu ya kila kitu kilichotokea ingawa kutokana na upasuaji aliofanyiwa anahitaji kupumzika saa 72,” alieleza Mhaville.
Mushi kuzikwa Uru
Mwili wa Mushi ambaye alijiua kwa kujipiga risasi,
unatarajiwa kusafirishwa na kuzikwa Kijiji cha Ongoma kilichopo katika
Kata ya Uru, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa kikao cha ndugu wa marehemu kilichofanyika kwenye Ukumbi wa 92 jijini Dar es Salaam jana, kaka wa marehemu, Silver Mushi alisema bado hawajaamua siku ya kusafirisha.
Alisema maandalizi ya mazishi yanaendelea na ndugu na jamaa zake wameshtushwa na taarifa za tukio hilo la mauaji kwani hawakuwa na taarifa zozote za mzozo baina yao na Julai mwaka huu marehemu na mzazi mwenzake huyo walisafiri pamoja hadi Uru mkoani Kilimanjaro.
Silver alisema kuwa wawili hao walikuwa wanapendana na kilichotokea kimewashangaza.
“Siwezi kusema kuwa walikuwa wachumba kwani katika mazingira yetu ya Kiafrika kuwa na mwanamke kwa miaka 10 hadi kuzaa mtoto mwenye umri mkubwa kama huo ni wazi kuwa nyie mna zaidi ya uchumba,” alisema.
Mushi alisema pia kuwa marehemu alikuwa anakaribia kuhitimu
Shahada ya Kwanza ya Masuala ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu Huria
nchini India.
Mushi awashtua wafanyakazi wenzake Darfur
Watu waliokuwa wakifanya kazi na Mushi kwenye Operesheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Kimataifa
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu jana, watu hao ambao waliwahi kuishi na Mushi wakiwa kwenye shughuli zao huko Darfur, walisema marehemu alikuwa na tabia ya upole, mcheshi na mchapa kazi.
Mfanyakazi mwenzake, ambaye ni raia wa Tanzania, ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa sio msemaji rasmi wa Unamid, alisema hakuwahi kusikia Mushi akinung’unika kuhusu masuala ya maisha yake.
Alisema pia mara nyingi, Mushi alikuwa akiwasiliana na mzazi mwenzake Ufoo nyakati za jioni. Walikuwa wakiwasiliana zaidi kwa njia ya mtandao wa intaneti.
“Kwa jinsi nilivyowaona kwa kweli walikuwa wanapendana sana. Kila mtu haamini kama kweli Mushi amefanya kitendo hiki cha kumpiga risasi Ufoo na kumuua mama mkwe wake,” alisema Mtanzania huyo kwa masikitiko makubwa.
Pia Mushi alikuwa anasifiwa kutokana na uwezo wake wa kufanya vitu vingi kiasi cha kupewa jina la utani la ‘multi talented’ (Mtu mwenye vitu vingi).
“Mushi akiwa hapa Unamid alikuwa kama mtaalamu wa mawasiliano lakini kumbuka huko nyuma aliwahi kuwa mpigapicha wa vituo vya televisheni vya ITV na TBC,” aliongeza raia huyo wa Tanzania, ambaye waliishi nyumba
moja katika Mji wa El-Jeneina huko Darfur ambako ni Magharibi mwa nchi ya Chad.
Mushi pia alikuwa ana sifa ya kupenda kula vyakula aina ya mboga na alikuwa analima bustani.
Mfanyakazi mwingine wa Unamid, ambaye ni raia wa Nigeria mwenye cheo cha Kanali, alisema Mushi alikuwa akilima mchicha, kabichi, bamia na mboga za majani ya maboga kwenye eneo la nyumba yake huko Darfur.
“Nani jamani ataangalia bustani ya Mushi?
“Siamini kama amefanya kitendo hiki,” alilalamika mtu huyo.
Polisi
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova amesema wanatarajia kutoa ripoti leo ya kupigwa
risasi kwa Ufoo na kuuliwa kwa mama yake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Kova alisema ripoti hiyo itatolewa na kamati waliounda kuchunguza suala hilo.
“Umma utaweza kuisoma, kuichambua na kutoa maoni kuhusu hatua za kuchukua ili matukio ya aina hiyo yasitokee tena,” alisema Kova.