Header ads

Header ads
» » KLABU ya Yanga imesema haina mpango wa kumrejesha Joseph Zuttah kwao

 Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha.
KLABU ya Yanga imesema haina mpango wa kumrejesha Joseph Zuttah kwao, isipokuwa wanaendelea na mazungumzo na baadhi ya timu za Zimbabwe kuona kama zitamchukua.
Akizungumza Dar es Salaam juzi Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema ni mapema kuzitaja timu zinazomtaka, kwani anasubiri kumaliza mazungumzo na timu husika kisha wataweka wazi.
“Hatuna mpango wa kumrejesha, tunafanya dili na tunasubiri wakati wowote likikamilika tutawaambieni kuwa ni timu gani, tunataka aendelee kuonekana katika timu,” alisema. Zutta alijiunga na Yanga kabla ya michuano ya Kagame ambapo alionekana kutokuwa na kiwango chenye ushindani na hivyo uongozi wa mabingwa hao wa bara ukaamua kuachana naye licha ya kuwa ilishasaini naye mkataba.
Mchezaji huyo tayari ameondolewa kwenye hesabu za kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara huku nafasi yake ikichukuliwa na Vincent Bossou wa Togo ambaye yupo nchini. Dk Tiboroha alisema kwa sasa mchezaji huyo ataendelea kuonekana kwenye kambi yao Mbeya hadi dili hilo litakapokamilika.
Wakati huohuo, Yanga leo inashuka kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuchuana na Mbeya City katika mchezo wa kirafiki. Mchezo huo utakuwa ni wa tatu tangu waende kujificha katika kambi yao iliyoko Tukuyu baada ya kushinda dhidi ya Kimondo FC ya Ligi Daraja la Kwanza mabao 4-1 na wa pili wakafunga 2-0 dhidi ya Prisons.
Mchezo huo ni wa mwisho wa kujipima nguvu kwa Yanga kabla haijarejea Dar es Salaam kuikabili Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa mwishoni mwa wiki ijayo.
Baadhi ya nyota wanaotarajiwa kuonekana katika mchezo huo wa kirafiki ni Malimi Busungu, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Amis Tambwe, Andrey Coutinho na Mateo Simon aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea KMKM ya Zanzibar.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema anatarajia baada ya mchezo huo wachezaji watakuwa wameimarika tayari kwa mchezo wao dhidi ya Ngao ya Jamii. “Mchezo huo ni muhimu kwetu kuendelea kuangalia viwango vya wachezaji wetu, nina imani kila mmoja ataonyesha nafasi yake uwanjani,” alisema.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post