WAKATI viongozi wa Yanga wakitimkia Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya usajili wa wachezaji watatu, Salum Mbonde ambaye ni mmojawao amesema atasaini Yanga.
Jana Jumanne, imedaiwa kuwa Yanga imetuma watu wawili Sauz kwa ajili ya kwenda kumalizana na wachezaji hao ambao wapo na kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kinachoshiriki michuano ya Cosafa nchini humo.Wachezaji hao ambao wanadaiwa pia kuwindwa na Simba, ni Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar, Haji Mwinyi wa KMKM na Said Ndemla aliyemaliza mkataba wake na Wekundu hao wa Msimbazi.
Hata hivyo, taarifa zilizozagaa mitaani kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa Ndemla tayari ameshamalizana na timu hiyo, kitu ambacho Yanga wamedai kuwa ni uzushi mtupu.“Baada ya hivi karibuni kumalizana na Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima, sasa tumeanza harakati za kukiongezea nguvu kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wa nje.
“Kuna viongozi wawili leo jioni (jana) wataondoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kumalizana na Mbonde, Ndemla na dogo mmoja hivi ambaye ni beki tatu wa timu ya KMKM ya Zanzibar anayeitwa Haji Mwinyi ambaye pia yupo Afrika Kusini na Stars.
“Dogo huyo ni mzuri, ana uwezo mkubwa na aliyempendekeza ni nahodha wetu Nadir Haroub ‘Cannavaro’,” alisema mtoa habari huyo huku akiomba kutotajwa jina lake gazetini kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa klabu hiyo.Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Katika hatua nyingine gazeti hili lilizungumza na Mbonde kwa njia ya simu kuhusiana na mpango wake huo wa kutua Yanga, akasema: “Bado mpango huo haujakaa sawa ila jinsi mambo yanavyoendelea kuna uwezekano mkubwa nikajiunga na Yanga kwa sababu wanaonekana kuwa tayari kutimiza mahitaji yangu kwa asilimia 90.”