Header ads

Header ads
» » John Magufuli Atangaza Kugombea Urais......Historia Yake kwa Ufupi Kuhusu Elimu yake na Uzoefu wa Kazi Viko Hapa


WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri huyo ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu mbio hizo za urais, kwa sasa ametangaza nia yake hiyo kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekwishatangaza rasmi ratiba ya mchakato wa urais kwa wanachama wake. 
 
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, ambaye ni mmoja wa mawaziri ambao kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo, anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura. 
 
Magufuli alitangaza azma yake hiyo muda mfupi nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana asubuhi, baada ya kukamilika kwa kipindi cha maswali na majibu. 
 
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia. 
 
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza. 
 
“Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,"alisema Dk. Magufuli. 
 
Alisema siku ya kuchukua fomu ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika hadhani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho. 
 
Kuingia kwake kwenye kwenye harakati za kuwania nafasi ya urais kunazidi kuufanya mchuano wa uchaguzi wa nafasi hiyo ndani ya CCM kwa mwaka huu kuwa mkali zaidi. 
 
Dk. Magufuli amekuwa mbunge tangu mwaka 1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah. 
 
Anajulikana kama kipenzi cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye mara kadhaa hakusita kumsifu hadharani, akimtaja kama mmoja wa ‘askari wa miavuli’ katika Baraza lake la Mawaziri. 
 
Aidha, uhusiano wake na Mkapa umejidhihirisha hadi kwenye masuala ya kifamilia ambako mara kadhaa Rais huyo mstaafu ameweza kuhudhuria hafla na misiba mbalimbali nyumbani kwa Dk. Magufuli. 
 
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Dk. Magufuli alipewa fursa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kusoma mafanikio ya chama hicho kwenye utekelezaji wa Ilani yake upande wa barabara. 
 
Uwezo wake wa kukariri takwimu mbalimbali ulikuwa kivutio kwenye mkutano huo na sehemu nyingine kama bungeni ambako hutakiwa kueleza mafanikio ya wizara yake. 
 
Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alimsifu kwa kumtaja kama ‘simba wa kazi’ kutokana na uchapaji kazi wake katika wizara mbalimbali ambazo ameziongoza. 
 
Kwa upande wa wananchi, wengi wanamuona Dk. Magufuli kama mmoja wa mawaziri wachapakazi waliowahi kutokea katika historia ya taifa letu. 
 
Hata hivyo, waziri huyo amekuwa akikosolewa kwa uamuzi wake wa uuzaji nyumba za serikali kwa watumishi na hata wasio watumishi wa umma. 
  
Pamoja na dosari hiyo, watetezi wake wanaamini kilichofanywa wakati huo na Awamu ya Nne kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri, na si uamuzi wa Dk. Magufuli mwenyewe. 
 
Magufuli ni nani?
Dk. John Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 Chato (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
 
Mwaka 1991 – 1994 alisoma shahada ya uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988 alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemiua na Hisabati. 
 
Mwaka 1981 – 1982: alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981 alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Juu ya Sekondari Mkwawa, Iringa. 
 
Mwaka 1977 – 1978 alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977 alisema Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera. 
 
Mwaka 1967 – 1974 alisoma Shule ya Msingi, Chato.
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma. 
 
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha. Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma. 
 
Uzoefu wa kazi
-Mwaka 2010 – hadi sasa; Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato. Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). 
 
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. 
 
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) Mwanza.
 
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati). 
 
Amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa. 
 
Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto kadhaa.

Imehaririwa na;- Unknown

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post