Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ambaye alianza kipindi chake cha kuongoza nchi mwaka 2005 kwa kuteua jumla ya mawaziri na manaibu 60, anaondoka akiwa ameteua jumla ya watu 118 kushika nyadhifa hizo, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.
Mwaka 2005 wakati akitangaza baraza lake la
kwanza, Rais Kikwete aliteua mawaziri 29 na manaibu 31, idadi ambayo
ilikuwa kubwa kulinganisha na marais waliopita, lakini alipofanya
mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, alipunguza ukubwa wa Serikali
baada ya kuteua mawaziri 26 na manaibu 21.
Hata hivyo, idadi kubwa ya watu walioteuliwa kuwa
mawaziri, imechangiwa na idadi ya mabadiliko aliyofanya tangu alipovunja
baraza mwaka 2008 kutokana na Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Ukijumlisha na mabadiliko hayo, tayari Rais
Kikwete amefanya mabadiliko makubwa ya mawaziri mara tatu na madogo
mengine mara tatu, hali inayoifanya Serikali yake kutumia mawaziri
tofauti 118 katika utawala wake hadi sasa.
Rais alifanya mabadiliko makubwa ya kwanza mwaka
2008 kutokana na kashfa ya mkataba wa Richmond iliyosababisha Lowassa
kujiuzulu na baadaye mwaka 2012 aliwaacha mawaziri sita kutokana na
kashfa iliyotokana na ripoti ya CAG, kabla ya kufanya mabadiliko mengine
makubwa mapema mwaka 2014 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza,
ambayo utekelezaji wake ulitawaliwa na uvunjaji mkubwa wa haki za
binadamu.
Katika kipindi hicho, mawaziri wanne walipoteza
maisha, mmoja alipata kazi Umoja wa Mataifa na wengine kujiuzulu na
hivyo kulazimika kufanya mabadiliko madogo manne.
“Mabadiliko haya ninayachambua katika sehemu
mbili. Kwanza, ili mtu aweze kufanya kazi kwa utulivu na kutekeleza
mikakati yake ni lazima awe na muda wa kutosha. Kama akikosa utulivu
taasisi (wizara) aliyopo inaweza kuyumba,” alisema Mkuu wa Shule ya
Sheria wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bonaventure Rutinwa.
Hata hivyo, Rutinwa, ambaye alikuwa mmoja wa
wasomi waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusu idadi ya mawaziri walioteuliwa
hadi sasa, alisema mara nyingi mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na
matatizo yanayotokea katika wizara zilezile, akitoa mfano Wizara ya
Nishati na Madini, ambayo alisema imesababisha wizara nyingine
kutetereka.
“Ili kuepusha jambo hili. Uteuzi katiza wizara
kama hii ya Nishati na Madini unatakiwa kufanywa kwa umakini zaidi ili
kuepuka kubadili mawaziri mara kwa mara,” alisema.
“Kama waziri anakuwa na mipango ya muda mrefu na akaondoka ndani ya kipindi kifupi, mambo yanaweza kukwama,” aliongeza.
Kwa upande wa pili, Profesa Rutinwa alisema
mabadiliko hayo huondoa fikra kwa baadhi ya mawaziri kuwa uwaziri ni
urithi badala ya nafasi hiyo kuwa ya kisiasa.
“Uwaziri utaendelea kuwa wako iwapo tu utafanya
vizuri kazi zako. Hata Rais Kikwete wakati akiingia madarakani aliwahi
kusema wazi kuwa yeye na Makamu wa Rais ndiyo wenye nafasi za kudumu, si
mawaziri aliowateua,” alisema.
CHANZO>>MWANACHI
CHANZO>>MWANACHI