Wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi CUF wanaokabiliwa na mashtaka matatu
ya kula njama na kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wameachiwa huru baada ya
kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa.
Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru jana aliwaachia huru washtakiwa hao
baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na
mdhamini mmoja anayeaminika na kila mdhamini asaini hati ya dhamana ya
maneno ya Sh 100,000.
Baada ya washtakwia hao kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu
aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 12,2015 kwa ajili ya kuangalia kama
upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Juzi, Mawakili wa Serikali, Joseph Maugo na Hellen Mushi, katika shtaka
la kwanza alidai kuwa Januari 27,2015 katika eneo la Temeke
washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya uhalifu.
Akisoma hati hiyo ya mashtaka, Maugo katika shtaka la pili alidai kuwa
siku hiyo ya tukio, washtakiwa 28 kati ya 30 wanaokabiliwa na kesi hiyo,
wakiwa katika ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke
bila ya kuwa na uhalali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya
maandamano kuelekea Mbagala Zakhem.
Katika shtaka la tatu, ambalo nalo pia linawakabili washtakiwa 28 kati
ya 30 , Wakili huyo wa Serikali, Maugo alidai kuwa siku hiyo hiyo ya
tukio katika eneo la Mtoni Mtongani waligoma na kutojali tangazo halali
lililotolewa na polisi lisilowaruhusu kuandamana na hata kufanya
mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hii ni Shabani Ngurangwa (56),
Shabani Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma Mattar (54), Muhamed
Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed(39), Abdul Juma(40),
Hassan Said (37), Hemed Joho (46) na Mohamed Ibrahim (31).
Pamoja na Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi Kaisi (51), Abdina
Abdina (47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma (33), Salehe Ally (43),
Abd Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally(32) , Said Mohamed
(40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Abdallah Said(45),Rehema
Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said (39).
Kwa upande wa washtakiwa Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37) wao
hawahusiki katika shtaka la pili na tatu ambayo yanawakabili wenzake.
SOURCE: MWANACHI