Dar es Salaam. Wakati CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa Ukawa, Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, imefahamika.
Tangu mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika
nyingi za kisiasa ndani ya vyama vya siasa na Jumanne iliyopita CCM
ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini Zanzibar na kutoa maazimio
yanayogusia mchakato huo lakini ikasita kutaja ratiba rasmi ya mchakato
wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na
kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini
Dar es Salaam Januari 20, ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano
wao, likiwamo suala la kupata wagombea huku vikao vya ndani ya vyama
vikitarajiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia
alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne akisema kutakuwa na
ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda
likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa
sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda nyingine alizotaja ni mwongozo wa Ukawa,
kura ya maoni ya Katiba, changamoto za uandikishaji wa daftari la
wapigakura, hali ya uchumi na tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliomalizika Desemba mwaka jana. Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi alisema watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta
majibu ya changamoto zilizopo kwa sasa.
Kiongozi huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila
chama ndani ya Ukawa kupitia vikao vyake kitateua majina ya wagombea
ambao watashindanishwa ndani ya umoja huo, akisema kabla ya Machi, jina
la mgombea urais ndani ya chama chake litakuwa limeshapendekezwa.
Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe alisema vikao vya chama hicho vinavyotarajiwa kufanyika
mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na ajenda ya uchaguzi vitakavyojadili
mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda yake inavyosema.
“Nadhani vikao hivyo ndiyo vitaanza kujadili
ajenda ya uchaguzi ujao. Tulishatoa nafasi ya watu kujitokeza kwenye
nafasi mbalimbali. Tukishapendekeza majina ya wagombea kwa baadaye ndiyo
tutawapeleka ili kuchambuliwa kwa pamoja na kamati ya Ukawa.
“Mpaka sasa kamati ya Ukawa inaendelea na kazi
yake tangu Oktoba mwaka jana ila inakuwa vigumu kwa wajumbe kujua kazi
zote zinazofanywa na kamati hiyo kutokana na msingi wa majukumu yake.”
Nyambabe alisema kamati hiyo imekuwa ikifanya
kazi, ikijumuisha wajumbe wasiopungua watatu kutoka kila chama ili
kufanya tathimini, kuchambua na kuratibu shughuli zote za uchaguzi.
Kuhusu kupata mwongozo wa Ukawa, Nyambabe alisema:
“Namna ya kupata mgombea, ilani moja na mwelekeo, vinaweza kuonekana
kuanzia Februari baada ya vyama kukaa vikao vyake.”
Wakati Nyambabe akisema hayo, kumekuwa na taarifa
katika vyombo vya habari kuwa CUF kimeshatangaza kumsimamisha Profesa
Ibrahim Lipumba kuwania urais, ambazo hata hivyo, zimekanushwa na Naibu
Katibu Mkuu wake Bara, Magdalena Sakaya.