Zanzibar. Wakati Kamati Kuu ya chama tawala, CCM ikimaliza vikao vyake mjini hapa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana amesema mambo mengi yanayozungumzwa kuhusu baadhi ya wanachama wanaotajwa kuwania urais hayana ukweli, wala hakuna atakayefukuzwa uanachama.
Kinana aliyasema hayo jana mjini hapa kuhusu mambo
yaliyojitokeza kwa wagombea wa nafasi za urais kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu, Oktoba.
Kamati Kuu ya CCM hadi jana jioni ilikuwa ikiendelea na kikao chake kwenye ofisi kuu ya chama, Kisiwandui, Zanzibar.
Kauli ya Kinana imekuja baada ya kuwapo kwa
minong’ono kuwa baadhi ya makada waliojitokeza kutangaza ama kuonyesha
nia kuutaka urais watachukuliwa hatua, zikiwamo kutimuliwa.
“Mambo yanayozungumzwa ni mengi kuwa baadhi ya
wagombea majina yao yatakatwa. Hayo ni majungu ya kisiasa, yamelenga
kuwachokoza viongozi na chama ili wapate cha kusema.
“Chama kina utaratibu na uamuzi unaofanyika kwa vikao maalumu, hizi ni propaganda, ni uchokozi kwa chama chetu,” alisema Kinana.
Wakati Kinana akijaribu kuwaondoa hofu vigogo
wanaowania nafasi hiyo, tayari wagombea hao wamepiga kambi mjini hapa,
baadhi yao wakiendesha kampeni za chini chini, tangu kumalizika kwa
sherehe za Mapinduzi visiwani hapa juzi.
Wagombea hao wamekuwa wakipishana kuingia visiwani
na kukutana na baadhi ya wajumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM na mkutano
mkuu kila upande ukijiimarisha kisiasa kabla ya mchakato wa kumpata
mgombea wa urais kupitia chama hicho Mei mwaka huu.
Vikumbo mitaani
Katika hoteli kadhaa mjini hapa baadhi ya makada
wamekuwa wakipigana vikumbo ikiwa ni hatua ya kuweka mikakati ya
kutengeneza mazingira, hasa ya kukubalika katika chama hicho.
Hata hivyo, tofauti na vikao vingine vya chama
hicho tawala, idadi ya wapambe wa makundi yanayotajwa kuwania urais
waliofika mjini hapa imekuwa ni ndogo