Vigogo
wa madawa ya kulevya wakiwemo viongozi wa dini sasa wanaanza kupukutika
kutoka kwenye mstari wa siri huku baadhi yao wakikimbilia nje ya nchi
kufuatia oparesheni kali inayofanywa na Kikosi cha Kupambana na
Kudhibiti Madawa ya Kulenya Tanzania kuwanasa kila kukicha, Uwazi lina
mchoro kamili.
Askofu Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria anayehusishwa na biashara ya madawa ya kulevya.
Hivi
karibuni kikosi hicho kimemkamata askofu (mwangalizi mkuu wa kanisa)
aliyetambulika kwa jina la Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria ambaye
ana kanisa la kiroho maeneo ya Sinza jijini Dar.
Jina la kanisa hilo limedhibitiwa na vyombo husika kwa sababu ya uchunguzi zaidi na uhalali wake wa kuwepo nchini.
SIKU YA TUKIO
Vyanzo
vyetu makini ndani ya kikosi kazi vinaeleza kwamba, mchungaji huyo
alikamatwa Oktoba 31, mwaka huu saa kumi usiku Tegeta wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya
heroine kilo 35.
KAMA UNGEINGIA SOKONI
Habari
za ndani kutoka kwenye oparesheni hiyo zinasema kuwa, endapo unga huo
ungeingia sokoni na kununuliwa, basi mtumishi huyo wa Mungu angevuna
kitita cha zaidi ya shilingi bilioni mbili.
NYUMBA ALIYONASIWA YA PROFESA
Mchungaji
huyo ambaye serikali imeanza kazi ya kulichunguza kanisa lake, alidakwa
na mzigo huo haramu kwenye makazi aliyopanga ambayo ni nyumba ya
profesa mmoja wa chuo kikuu, Mbezi jijini Dar es Salaam.
Askofu akiwa chini ya ulinzi.
WASHIRIKA NAO WADAKWA
Kwa
mujibu wa chanzo, kamatakamata ya mchungaji huyo pia iliwakumba
watuhumiwa wengine ambao ni Walyat Khan raia wa Pakistani, Chuksi
Sylvester Agbazuo na Tony Olafor wote raia wa Nigeria na inadaiwa kwamba
walikuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali na kutoroka.
HABARI NYETI
Habari
za siri ambazo Uwazi ilizinasa zinadai kuwa, watumishi wa Mungu
waliokuwa kwenye orodha ya kunaswa walikuwa wengi lakini wamekimbilia
nje ya nchi na kikosi hicho kimeshawasiliana na Polisi wa Kimataifa
(Interpol) kwa ajili ya kuwasaka na kuwatia nguvuni.
MAJINA MAPYA MEZAN KWA NZOWA
Taarifa
zaidi zinaeleza kwamba, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kupambana na
Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa amekabidhiwa
majina ya vigogo wakiwemo viongozi wa dini ambao ni sugu katika biashara
hiyo. Mbali na majina hayo, pia amepewa ratiba zao za safari za
kibiashara hivyo kilichobaki ni kuwafuatilia na kuwakamata na ushahidi
ili kuhakikisha kwamba hawawezi kupona mahakamani.
MTANDAO HATARI
Habari
zaidi zinadai kuwa, siku za hivi karibuni, Kamanda Nzowa amekuwa
akifumua mtandao wa watu wazito katika biashara hiyo na imebainika kuwa
vigogo hao wana mtandao mkubwa serikalini ikiwemo wizara ya mambo ya
ndani ambao wanawalinda kwa kupewa mamilioni ya pesa kwa ajili ya
usimamizi wa upitishwaji wa biashara hiyo haramu kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar.
“Unajua
zamani viongozi hao serikalini walikuwa wakimsumbua Kamanda Nzowa ili
awaachie watuhumiwa waliokamatwa na unga bila mafanikio, lakini sasa
wameshamsoma kiasi kwamba hata wakikamatwa hawampigii simu tena,”
kilisema chanzo kingine.
Dawa za kulevya alizokutwa nazo askofu huyo.
WATOTO WA VIGOGO
Habari
nyingine zinadai kuwa, Kamanda Nzowa pia ana majina ya watoto wa vigogo
wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo na anayafanyia kazi.
KUMBUKUMBU
Kukamatwa kwa askofu huyo kumekuja baada ya kukamatwa kwa vigogo ambao ni viongozi wa dini katika makanisa ya kilokole.
Januari
11, mwaka huu, Askofu Moris Charles alidaiwa kukamatwa na polisi maeneo
ya Chinga Mbili mkoani Lindi akiwa na kilo 210 za madawa ya kulevya
aina ya heroine yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4, kesi yake bado
inaendelea mahakamani mkoani humo.
Juni
8, 2011 polisi walifanikiwa kumkamata Mchungaji Kapupu Denis Okechuku
wa kanisa la kilokole lililopo Kinondoni Biafra akiwa na kilo 81 za
cocaine, kesi yao bado ipo Mahakama ya Kisutu, Dar.
Nyumba aliyokutwa askofu huyo.
KAMANDA NZOWA
Uwazi
lilipomtafuta Kamanda Nzowa ofisini kwake juzi, alisema kuna watu wanne
waliokamatwa Tegeta wakiwa na kilo 35 za madawa ya kulevya aina ya
heroin na kuna wengine wanatafutwa kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa
sasa nisingependa kuzungumzia sakata hilo kutokana na sababu za
kiupelelezi kwani kuna wengine tunawatafuta na nitahakikisha wanakamatwa
na kufikishwa katika vyombo vya sheria, nawashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao,” alisema Nzowa.
CHANZO GPL