Wakati jua likichomoza katika delta ya mto Nile, wafanyakazi katika shamba la samaki kaskazini mwa Misri wanafungua mlango na kutenganisha maelfu ya samaki aina ya sato ambao wanamwagwa katika tenki. Samaki wanatenganishwa, wanafungwa katika viroba na kupelekwa katika masoko murua (supermarkets) katika jijiji la Cairo na Alexandria, ambako wanauzwa kama "samaki waliovuliwa siku hiyo".
CAIRO, Nov 1 (IPS) - Misri imejenga sekta kubwa ya uvuvi barani Afrika, na kuwa na mashamba manne katika kila mashamba matano ya samaki katika bara. Mashamba ya samaki ya Misri yalizalisha zaidi ya tani 650,000 za samaki mwaka jana, au asilimia ipatayo 60 ya samaki wa maji baridi na maji chumvi waliozalishwa nchini humo, na kuchangia protini ya bei nafuu kwa wakazi milioni 80 nchini humo.
"Kukua kwa kiasi kikubwa kwa uvuvi kumefanya samaki kuwa nafuu kununulika kwa wakazi wengi wa Misri, hivyo leo hii samaki na bei ya kuku inakaribia kuwa sawa kwa kilo," anasema Malcolm Beveridge, Mkurugenzi wa Kituo cha Ufugaji wa Samaki na Jenetiki katika Kituo cha Samaki cha Kimataifa. "Inaonekana kana kwamba wengi wa walaji wanabadilisha kati ya aina hizo mbili, ikitegemeana na kile kinachouzwa bei nafuu zaidi."
Mashamba ya samaki ya biashara nchini Misri yaliongezeka miaka ya 1960 katika pwani ya maziwa na wangwa za bahari. Sekta hiyo imeshuhudia kukua kwa kasi katika muongo uliopita. Jumla ya uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia 500 tangu mwaka 1998 kutokana na kutumia njia za ufugaji wa kisasa na aina ya samaki wanaokua kwa kasi zaidi kama vile sato.
Mamlaka Kuu ya Maendeleo ya Rasilimali Samaki (GAFRD) inajipanga kuendeleza zaidi uvuvi wa samaki nchini humo, na imeweka lengo la kufuga tani milioni 1.1 za samaki, au asilimia zipatazo 75 za jumla ya uzalishaji wa samaki, ifikapo mwaka 2012. Ni mkakati wenye pande mbili wenye lengo la kuongeza uzalishaji wa samaki wa maji baridi, wakati huo huo ukihamasisha uwekezaji katika ufugaji wa samaki wa maji chumvi.
Rasilimali chache za maji baridi nchini Misri ni kikwazo kwa maendeleo haya. Nchi ambayo kwa kiasi kikubwa ni jangwa inategemea Mto Nile kwa asilimia 95 kwa ajili ya mahitaji yake ya maji, na matumizi ya maji yanaoenekana kama suala la usalama wa taifa. Kipaumbele kinatolewa kwa maji ya bomba na umwagiliaji, na kuacha zaidi ya asilimia 90 ya mashamba ya samaki kuendeshwa katika mifereji inayotumika kwa kilimo cha mazao.
"Siyo wazo zuri kutumia mifereji ya kumwagilia mashamba ya mimea kwa ajili ya kuzalishia samaki, kwasababu pamoja na kuwa na lishe nyingi ndani yake, pia kuna mabaki ya madawa ya kuulia wadudu, na hii ina uwezekano wa kusababisha hatari kwa walaji," anasema Beveridge. "Hakuna mantiki kufanya ufugaji wa samaki kutumia kwanza maji, na kuiruhusu mifereji ya wafugaji wa samaki kutumiwa na wakulima wa mazao."
Sheria zilizopitishwa karne iliyopita zinazuia miradi ya uvuvi wa samaki kutumia maji ya juu ya ardhi, lakini mwanya unasababisha wafugaji wa samaki kuanza kutumia maji ya chini ya ardhi. Wakulima wanaweza kusukuma maji safi kutoka chini ya ardhi na kuyaingiza kwenye mabwawa, na kutumia mifereji yenye lishe ya kutosha kurutubisha na kumwagilia mashamba ya mazao – mfumo wa jumla wa uzalishaji wa chakula.
Mfumo huo tayari unatumika katika shamba la majaribio la Wadi Natroun, eneo la ukanda wa chini umbali wa kilomita 110 kaskazini magharibi mwa Cairo. "Mradi wa majaribio unatumika kama mfano wa wakulima wanaofanya kazi katika jangwa juu ya jinsi ya kuongeza uzalishaji wao na kipato kwa kutumia kiasi cha maji kama hicho kwa malengo mawili, au matatu," anasema mwenyekiti wa GAFRD Mohamed Fathy.
Njia hiyo inahusiana na kuzungusha rutuba na kusaga taka, anasema. "Kwanza, mkulima anasukuma maji ya chini ya ardhi katika mabwawa kwa ajili ya kufuga sato na kambare. Maji kutoka madimbwi ya kambare yanatumika kumwagilia majani ya alfalfa, na katika mashamba haya kondoo na mbuzi wanalishwa majani haya. Mbolea inayotokana na mifugo inatumika kwa kuzalishia umeme wa kinyesi, ambao unatumika kuongeza joto la maji kwa ajili ya kuzaliana kwa sato, au kuleta joto kwa ajili ya samaki katika madimbwi wakati wa majira ya baridi kali."
Ufugaji wa samaki pamoja na mifugo mingine kwa sasa unachangia kiwango kidogo cha uzalishaji wa samaki nchini Misri sasa, lakini sehemu yake inatarajiwa kuongezeka kwa kasi kubwa. Fathy anaona fursa kubwa iliyopo kwa mbinu hiyo kuongeza uzalishaji wa chakula katika eneo kubwa la ardhi ya jangwa ambayo imetengenezwa kuweza kuzalisha.
GAFRD inashiriki katika miradi kadhaa ya kuongeza uzalishaji wa samaki, ikiwa ni pamoja na kuendeleza maeneo ya kuzaliana, utafiti wa kijenetiki na programu za kuzaliana. Inatarajia kuongeza wastani wa uzalishaji kwa mwaka wa samaki kutoka mashamba ya maji baridi hadi tani 5 kwa ekari, kutoka wastani wa tani 1-3 kwa ekari.
Shirika hilo pia linajaribu kukuza ufugaji wa samaki wa maji ya chumvi, ambao kwa sasa unachangia asilimia 5 ya jumla ya samaki wote wanapozalishwa. Mashamba ya samaki wa maji chumvi tayari yanazalisha changu, kamba wadogo, ngisi na samaki wengine wa maji chumvi, na GAFRD imetanga maeneo ya pwani kwa ajili ya kuendeleza maeneo ya ufugaji na mashamba ya ufugaji wa samaki kandokando mwa bahari.
Uchaguzi wa aina ya samaki utakuwa jambo muhimu kwa mafanikio ya kibiashara ya miradi hii, wanasema wataalam. Waendeshaji wa ufugaji wa samaki wa maji chumvi lazima wazingatie gharama za kufuga samaki, kiwango cha ukuaji, mahitaji ya nafasi na mahitaji ya soko.
Samaki wanaokula mimea kama vile ngisi wanaopendwa mno ndani ya nchi, lakini lazima wafugwe katika mdimbwi ya kina kifupi yenye eneo kubwa. Kwa kulinganisha, aina nyingine ya samaki wanaweza kufugwa katika vizimba au matenki, lakini wanahitaji chakula cha gharama kubwa na hivyo kuongeza gharama.
"Kupata ardhi nchini Misri siyo rahisi sana na hii ni kutokana na ushindani wa utalii na kilimo, na hii ndiyo sababu ufugaji wa maji chumvi unapendelea aina nyingine ya samaki ikilinganishwa," anasema Sherif Sadek, mshauri mtaalam wa ufugaji wa samaki nchini humo. "Tunachohitaji ni samaki wanaopendwa zaidi ambao tunaweza kuwafuga katika mazingira ya bahari bila ya kuwa na haja ya kuwalisha chakula chenye protini kubwa. Kama sivyo nina wasiwasi samaki hao wanaweza kuwa wa kuuzwa nje tu au kuliwa na watu matajiri."
Kupanuliwa kwa uzalishaji wa vifaranga wa sato, ambao wanatumiwa zaidi na wazalishaji wa sato nchini Misri, kumepunguza gharama ya kuhifadhi samaki wengi wa maji baridi ikilinganishwa na muongo uliopita. GAFRD kwa sasa inatoa leseni za vitalu vya kuzalishia vifaranga wa samaki wa maji chumvi, ambako – ikiwa ni pamoja na kupanuka kwa viwanda vya samaki – kunatarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji.
Mshindi halisi, wanasema wataalam, ni mlaji wa Misri. Kukua kwa sekta ya ufugaji wa samaki kumesababisha kushuka kwa bei ya reja reja ya samaki, jambo ambalo kwa kiasi limehamasisha wananchi wa Misri kuongeza samaki zaidi katika mlo wao. Matumizi ya samaki kwa kila mwananchi kwa mwaka yameongezeka mara mbili tangu mwaka 1995 na kufikia karibu kilo 14, na sasa samaki wanachangia zaidi ya asilimia 20 ya matumizi ya
protini inayotokana na wanyama.
CHANZO CHA HABARI
Ni kwa msaada wa Inter Press Service News Agency
UNGANA NAMI FACEBOOK