Header ads

Header ads
» » UKITEGEMEA MSHAHARA TU, KUFANIKIWA UTASUBIRI SANA!-2

NICHUKUE nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kila jambo ambalo amekuwa akinitendea katika maisha yangu. Amenijalia afya njema, nguvu za kutosha lakini pia amenipa uwezo wa kuandika yale ambayo yameonekana kuwa ni yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Aidha, niwakumbushe tu kwamba, kama una jambo lolote linalokusumbua katika maisha yako, usisite kuwasiliana nami kupitia simu yangu ya mkononi kwa namba zilizopo hapo juu. Kumbuka kwamba, unapojilimbikizia matatizo mengi kichwani mwako ambayo hujayapatia ufumbuzi ‘Accumulation of unsolved problems’, unaweza kuumwa na hata kuyafupisha maisha yako.
Ndugu zangu, wiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu. Nilianza kuzungumzia suala la mshahara hasa kwa wale ambao wameajiriwa. Nikasema, ukitegemea siku moja utakuwa miongoni mwa waliofanikiwa kwa kutegemea mshahara, utasubiri sana.
Wapo walioonesha kunielewa na wengi kufikia hatua ya kutoa ushuhuda wa jinsi walivyokuwa nyuma kimaendeleo wakati walipokuwa wakitegemea mshahara tu na mafanikio waliyoyapata baada ya kuanzisha vyanzo vingine vya mapato.
Huo ndiyo ukweli wenyewe! Hakuna siku mshahara utatosha na kukufanya wewe ufanye mambo ya kuonekana kwenye jamii. Mwisho wa siku utajikuta unakula, unavaa na kulala pazuri lakini hakuna kingine cha maana utakachokifanya.
Waliobahatika kusoma makala ya wiki iliyopita baadhi waliamua kunipigia simu na kutaka kujua ni kipi wanaweza kukifanya ili kuanzisha kipato kingine. Wengi walieleza kuwa, wanatamani sana kuwa na vyanzo vingine vya mapato lakini wanashindwa kutokana na kutokuwa na mtaji lakini pia muda unawabana kufanya mambo mengine kwa kuwa wameajiriwa.
Kwanza kabisa, unatakiwa kuweka akilini mwako kwamba unatakiwa kuwa na kitega uchumi kingine mbali na kazi yako ya kuajiriwa. Ukishaliweka hili akilini mwako, hakikisha unajiwekea malengo kwamba kutoka kwenye mshahara wako ‘unasevu’ pesa ambayo baada ya muda itakufanya upate mtaji wa kuanzisha biashara nyingine.
Biashara hiyo inaweza kuwa ya genge, duka, saluni, ufugaji wa kuku au nyingine utakayoona inafaa. Baada ya kuianzisha biashara hiyo, kama mkeo hana kazi unaweza kumpa jukumu la kuiangalia au muajiri mtu atakayeisimamia wakati wewe ukiendelea na ajira yako kama kawaida.
Kama utashindwa ‘kusevu’ pesa kutoka kwenye mshahara wako kutokana na matumizi ya kifamilia kukubana, angalia uwezekano wa kutafuta mkopo kutoka kwenye taasisi za fedha.
Ukiona nako kuna ugumu, zungumza na ndugu, jamaa na marafiki zako ambao wana uwezo kidogo. Washirikishe kwenye wazo lako, naamini wanaweza kushawishika kukukopesha na hatimaye kuanzisha biashara uliyoiwaza.
Weka tu akilini mwako kwamba kamwe mshahara unaopata hauwezi kutosha hivyo una kila sababu ya kuangalia uwezekano wa kuwa na vyanzo vingine vya pesa ili siku moja uwe kati ya watu wenye mafanikio makubwa.
Pia kumbuka wengi unaowaona wenye mafanikio makubwa, hawakutegemea chanzo kimoja cha fedha. Walijitahidi kuanzisha vyanzo vingi vya mapato na wakawa na nidhamu na kila shilingi waliyoipata wakielewa kwamba, hata kama utakuwa na vyanzo vingi vipi, kama hutakuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha zako, kamwe huwezi kufanikiwa.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post