Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeziagiza kampuni za simu kuanzisha vifurushi vinavyotenganisha huduma za inteneti, sauti na meseji ili kuwapatia machaguo wananchi na kuwapunguzia gharama zisizo za lazima.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba amesema hayo wakati wa
ufunguzi wa semina kwa walimu wa uziwi. Agizo hilo lililowahi kutolewa
awali mapema mwaka huu litafanya kampuni hizo kuweka vifurushi rafiki
kutokana na mahitaji ya mtumiaji.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa mdhibiti huyo, ilitokana na kuwepo
malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kushushwa ghafla viwango vya
huduma katika vifurushi vingi vya mitandao ya Vodacom, Tigo na Airtel
mapema mwaka huu.
“Vifurushi vingi vinajumuisha huduma ambazo baadhi ya watumiaji
hawahitaji. Mfano, mtumiaji mwenye uziwi anahitaji zaidi kifurushi cha
meseji zaidi kuliko sauti. Mtumiaji asiyeona anahitaji zaidi kifurushi
cha kuzungumza kuliko meseji.
“Hivyo mamlaka imeagiza kampuni kuvitenganisha vifurushi kwa mahitaji ya mtumiaji,” amesema Dk Simba.
Amesema baada ya agizo TCRA imekuwa ikifuatilia kwa karibu
utekelezaji wake na kwamba baadhi ya kampuni zimeshaanza kutenganisha
vifurushi hivyo kama ilivyoamriwa.
Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa Sheria ya kudhibiti uhalifu
mtandaoni ya mwaka 2010, Dk Simba amesema kuwa TCRA imekuwa ikipokea
maombi mengi kutoka jeshi la polisi kutoa ushahidi wa kesi mbalimbali
zinazohusu uhalifu mtandaoni.
Amesema katika utekelezaji wa sheria hiyo iliyoanza Septemba Mosi
mwaka huu, wamekumbana na changamoto ya baadhi ya watu kukosea na
kupeleka malalamiko yao moja kwa moja TCRA badala ya polisi ambao wana
mamlaka ya kisheria kufungua kesi za jinai.
“Tangu kuanza kwa sheria hiyo nidhamu ya matumizi ya mtandao imeanza
kuimarika japo wapo baadhi wanaendelea kuvunja sheria. Hata hivyo,
kumbuka hata tukipata ushahidi ni suala la polisi kuendelea au
kutoendelea na kesi,” amesema Dk Simba.