Watu 32 wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kupigwa na umeme wa radi katika mikoa ya Andra Pradesh na Orissa mashariki mwa India.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya India, watu 23 walifariki katika miji mitano iliyoko viungani mwa mkoa wa Andra Pradesh, huku wengine 9 wakifariki mkoani Orissa.
Watu wengine 12 waliojeruhiwa kutokana na umeme wa radi pia wameripotiwa kufikishwa hospitalini.
Wengi wa watu hao waliokumbwa na maafa ya umeme wa radi wanasemekana kwamba walikuwa wakifanya kazi mashambani.
Wanawake wawili kati ya majeruhi walipigwa na umeme wa radi uwanjani wakati wa mechi ya mchezo wa kriketi katika mji wa Guntur ulioko mkoani Andra Pradesh.
Waziri Mkuu wa mkoa Chandrababu Naydu, ametangaza kwamba serikali itatoa malipo ya fidia ya Rupee 400,000 kwa kila familia ya watu waliopoteza maisha.
Msimu wa mvua za Monsoon huanza kati ya mwezi Juni hadi Septemba kila mwaka nchini India na umeme wa radi unapiga husababisha vifo vya watu wengi.