TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetahadharisha wanasiasa, kuacha mara moja kutumia kauli ambazo zinaweza kuwa chanzo cha kuhatarisha amani ya nchi katika mikutano yao ya kampeni.
Pia, tume hiyo imetahadharisha wanasiasa kuwa wale watakaoendelea kutoa kauli hizo, zitakazozua chuki na kisha kuleta machafuko katika nchi, wanaweza kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alitaja kauli hizo kuwa ni “Serikali tukiibiwa kura patachimbika”, “Ushindi ni lazima”, “Serikali haitolewi kwa vikaratasi”, “Goli la mkono au ushindi saa nne asubuhi”.
“Kauli kama hizi zinajenga hisia ambazo zinaweza ku-undermine process (kudumaza mchakato) yaani mchakato mzima wa uchaguzi,” alisema Nyandunga wakati akizindua Ilani ya Uchaguzi ya asasi za kiraia kuelekea na baada ya Uchaguzi Mkuu. Uzinduzi huo ulifanyika Dar es Salaam jana.
Pia tume hiyo ilitoa tahadhari kwa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kuhusu uwepo wa vikundi vya ulinzi ndani ya vyama vya siasa.
Ilisisitiza kwamba uwepo wa vikundi hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi. Nyanduga alisema uzoefu unaonesha kuwa katika nchi mbalimbali, vikundi kama hivyo vimekuwa vyanzo vya vurugu na uvunjifu wa haki za binadamu, hasa baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika, pasipokuwepo uwazi na haki.
Alisema vikundi hivyo, haviwajibiki kwa mujibu wa sheria kwa mtu yeyote, bali vinalinda maslahi ya vyama. Alisema vikundi hivyo hutumika vibaya, pale wanasiasa wasipokubaliana na matokeo.
“Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaitaka Serikali kupiga marufuku vikundi hivyo kujihusisha kwa namna yoyote ila na mchakato wa uchaguzi, ikizingatiwa kwamba Jeshi la Polisi limeimarishwa kutoa ulinzi kwa wagombea, wananchi na mali zao,” alieleza Mwenyekiti huyo.
Nyanduga alitaka tume za uchaguzi, zihakikishe kuwa taratibu zote za Uchaguzi Mkuu zinaendeshwa kwa uwazi, haki kwa misingi ya sheria na taratibu za uchaguzi.
Alivitaka vyama vya siasa, kama wadau wakuu washirikiane na tume za uchaguzi katika hatua zote hasa wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.