MIAKA tisa iliyopita Terry Dean Baucom alikuwa muuzaji wa
magazeti katika barabara za Jimbo la Michigan nchini Amerika. Lakini kwa
sasa, Bw Baucom mwenye umri wa miaka 49 ni muuzaji wa mandazi katika
mitaa ya mji wa Siaya, eneo la Nyanza.
Kwa siku tano kwa wiki, Bw Baucom huchuuza mandazi na bisi (mahindi yaliyokaangwa) akitumia baiskeli.
Tangu alipowasili Siaya mnamo Agosti
2014 pamoja na mkewe na binti zake watatu, Bw Baucom amejifunza lugha
ya Kidholuo na ana uwezo wa kuzungumza lugha hiyo japo maneno kadhaa
humtatiza.
“Amosi (hali gani?)” aliamkua waandishi wa Taifa Leo wakati walipokutana naye ili kumhoji.
Bw Baucom na familia yake wanaishi
katika mtaa wa Banana viungani mwa mji wa Siaya. Alisema kuwa alijitosa
katika biashara ya kuchuuza bidhaa hizi kama njia nzuri ya kuwashawishi
wakazi wa Siaya kusaka na kupata fedha za kusaidia wasiojiweza.
Bw Baucom huuza mandazi, bisi na keki katika maduka ya jumla na yale madogo madogo.
Wakazi wa Siaya wanasema kuwa keki
anazotengeneza Baucom ni za kipekee kwani huwa na ladha tofauti tofauti
kama vile 'vanila’ na ndizi.
“Nilianza kazi hii kwa sababu wasio
na chochote katika jamii wamepuuzwa na matajiri, kando na kutoheshimiwa
na wengi,” akasema Bw Baucom.
Alisema hufanya biashara hiyo kwa
madhumuni ya kusaidia watu maskini katika kanisa lake la New Covenant
Outreach World ambalo lina makao makuu nchini Amerika.
Bw Baucom alisema wenyeji wa eneo
hilo wanashangaa kuona raia wa Amerika akijihusisha na uchuuzi lakini
azma yake ya kusaidia wasiojiweza humpa motisha kila siku.
Kuhubiria watu
“Japo biashara hii haina faidi
kubwa, ninapata mapato ya kutosha kukimu mahitaji ya familia yangu na
pia kusaidia maskini katika jamii,” aelezea Bw Baucom.
Anapowauzia wateja wake bidhaa hizi, Bw Baucom, vilevile, huwahubiria mafunzo ya Kikristo.
“Kama Mkristo, ni muhimu kuwa na
moyo mkunjufu. Natumia biashara yangu kuinua kanisa na kuwapa moyo
maskini pamoja na kufadhili elimu ya watoto mayatima mjini Siaya,”
akaeleza.
Bw Baucom alisema kuwa kwa siku
anapata faida ya Sh2, 000 na kati ya fedha hizo, hutoa Sh500 kwa
shughuli za kanisa hilo la New Covenant Outreach lililoko katika
barabara ya Siaya-Ndere.
“Huwa ninatoa kati ya Sh300 hadi 500
kila siku kwa shughuli za kanisa kulingana na faidi ambayo nimepata kwa
siku,” alieleza Bw Baucom.
Kwa usaidizi wa binti zake na mkewe, amefanikiwa kuongeza mapato yake kwa sababu wanasambaza bidhaa zake kwa wateja zaidi.
Katika siku za wikendi, familia ya
Bw Baucom hutembelea wafungwa katika jela ya Siaya na wagonjwa katika
Hospitali Kuu ya Kaunti ya Siaya, kuwafanyia maombi.
Bw Baucom alizaliwa katika Jimbo la Michigan na akahamia Ufilipino mnamo 1997 baada ya kuacha kazi yake ya kuuza magazeti.
Alianzisha kanisa la New Covenant Outreach World mnamo 2009 na akatumwa Kenya mnamo Agosti 2014.