Licha ya umaarufu wake, Hifadhi ya Taifa Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha ina mambo mengi ya kuvutia yanayoifanya muda wote kuwa ya kipekee duniani.
Upekee huo unatokana na mfumo wa maisha ya binadamu yanavyohusiana moja kwa moja na maisha ya wanyama.
Siyo jambo geni kusikia kuwa binadamu hasa wa
jamii ya Kimasai wanaoishi kwenye eneo la hifadhi hiyo wanaishi na
mifugo yao katika maeneo yaliyo na wanyamapori bila kudhuriana.
Hata hivyo, jambo linaloweza kuwa geni na la ajabu
ni baadhi ya koo za Kimasai ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuelezwa
kwamba ‘zina udugu’ na baadhi ya wanyama.
Licha ya maelfu ya watalii kutembelea hifadhi hiyo
ili kufaidi na kuona wanyama waliosheheni Ngorongoro, kasi ya wageni
hao pia ni kubwa kutembelea jamii ya Wamasai inayoishi eneo hilo ili
kujua mila na tamaduni zao na namna wanavyoweza kuishi na wanyama.
Hakika hakuna ubishi kwamba Wamasai wa Ngorongoro na wanyama katika Hifadhi ya Ngorongoro ni marafiki.
Ukweli huo unakwenda mbali zaidi na kubainisha
kuwa hata baadhi ya koo za Kimasai, ‘zina udugu’ na wanyama kwa kadri
ya majina yao.
Inaelezwa kuwa kuna ukoo wenye ‘udugu’ na nyoka, mwingine simba hata wanyama wengine.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), Vincent Mbilika anaeleza kuwa zipo koo ambazo majina yao yana
uhusiano na wanyama hata wadudu.
Mfano; ukoo wa Mollel unatajwa kuhusiana na faru,
Laitayok unahusiana na tembo na mbogo, nyani na tumbili wanahusianishwa
na ukoo wa Ilukumai, ambao fisi na nyoka wanaelezwa kuwa na uhusiano na
ukoo wa Illtarru-sero.
Mbilika anaeleza kuwa katika koo iliyo ndugu na
nyoka, jamii hiyo ikikuta nyoka ndani ya nyumba yao haipambani naye
tofauti na ilivyo kwa jamii nyingine, zinachofanya ni humwekea maziwa
kwa kumwagia, naye huyanywa.
“Baada ya kupewa maziwa, hutoa ndimi zake na
kulamba maziwa kisha hutoka ndani ya nyumba bila kudhuru mtu, tena
anatokea mlangoni. Hivyo, koo yenye udugu na nyoka hata kama ni mkubwa
kiasi gani, ikiwa ameingia ndani ya nyumba, hata kufikia hatua ya
kulala kitandani na mtoto mdogo, hauawi,” anasema Mbilika.