Unapozungumza na watu karibu wote duniani, kila mtu atakwambia ninachotaka ni kuwa na maisha bora.
Huenda ni jambo lisilowezekana mtu kusema kwamba anataka kuwa na maisha ya shida, kama atakuwepo basi huenda mawasiliano kwenye ubongo yakawa yameingizwa na shida; tunaweza kusema hawa ni aina ya watu maalumu wanaohitaji msaada maalum...teh!teh!teh!
Unaweza kuringa una shahada, stashahada na elimu zingine, bado ukawa unachapwa bakora na maisha kama hutakuwa makini; Kusoma sana au kidogo, kuwa na rafiki waliofanikiwa au wasiofanikiwa, kwenda nje ya nchi au la, au kuzaliwa familia maskini au tajiri, bado sio tiketi ya kukufanya uwe na maisha bora.
Msingi wa kufanikiwa ni kuthubutu kufanya jambo fulani, kwa mfano kufungua mradi na mambo mengine kama haya. Kuna watu kwa mfano unaweza kuona anakata tamaa kwa sababu labda amezaliwa katika familia maskini, kitu ambacho sio sahihi. Msingi wa kuwa na maisha bora ni kufanya kazi kwa bidii na zaidi ni kuishi kwa malengo; Usiishi tu ili mradi siku zinakwenda mbele. Kwa chochote unachokifanya, kifanye baada ya kutafakari na kuangalia faida au hasara yake.
Katika kitabu changu cha mwongozo wa namna ya kutengeneza bidhaa zikiwemo sabuni, mishumaa, vyakula vya kuku nk, nilisema maisha yanatuhitaji kuwa waangalifu na wanadamu wanaotunguka, lakini pia ni lazima tubuni miradi mingi zaidi ili tuweze kufanikiwa kuwa na maendeleo.
Kuna mwingine hata ukimwangalia sura yake anaonekana wazi kabisa kwamba hana furaha, unapomwambia kwamba mambo yangu yanakwenda safi. Furaha ya watu walio wengi ni kusikia unaishi maisha ya kawaida, au unaishi maisha ya shida.
Kwa bahati mbaya sana, siku hizi hadi baadhi ya wazazi wamekuwa wabaya kwa watoto wao, kuna wengine kwa mfano hajui ni kwa vipi unaendesha gari, unaishi nyumba nzuri, badala yake anapokuona unaendesha gari zuri anakuja juu na kulalamika kuwa mbona huwasaidii.
Ambacho nataka kusisitiza katika makala haya ni kwamba mafanikio yako yanatokana na akili yako uliyonayo, ndio maana wengine wamekuwa wakisema kuwa ‘ugumu wa maisha ndio kipimo cha akili’.
Wengi wanapingana na msemo huu, lakini ndio ukweli wenyewe kwamba hali ya maisha ambayo unayo, ndio hasa inayoeleza hali ya uwezo wa kufikiri. Endapo utatumia akili, hisia na imani yako kwa busara na kufanyia kazi, ni lazima maisha yako yatakuwa na mabadiliko makubwa.
Kama wewe ni mwanaume, hebu tuseme ule ukweli unafanya ngono na wanawake wangapi? Unawahonga kiasi gani au unatumia kiasi gani kwa ajili ya mambo yasiyo na maana? Jibu unalo, kama unapanda fedha zako kwenye kuhonga, kisha unatarajia maendeleo, bila shaka akili yako haiko sawa; watu huvuna wanachopanda, si ndiyo?
Katika kitabu cha tiba ya ndoa ambacho ni maalum kuhusu namna ya kuishi kwenye ndoa nilifafanua namna gani wanapaswa kufanya ili mwenzi wako asikuchoke au namna gani ufanye ili kuifanya ndoa yako iwe ya maana; Mtu huvuna kile alichopanda, si ndio jamani? Kama unaelekeza fedha nyingi kwenye kitu fulani, hakuna ubishi kwamba mwisho wa siku utavuna matunda ya kile kitu ambacho umewekeza fedha zaidi.
Unaweza kumficha mkeo asijue una wanawake ulionao, lakini amini ninachokwambia hakuna ujinga uliopitiliza duniani kama kufanya ngono hovyo na kukubali kutumiwa kama mashine ya kutolewa fedha; badala ya kuendeleza kwako unakuwa mjinga wa kuhonga wanawake kisa wanakupa nanilihii.
Tangu umeanza kufanya umepata nini? Jibu unalo mwenyewe; amini ninachokwambia ni ngumu kwako kufanikiwa kama unaendekeza mambo ya ajabu. Je, maisha yako unayaendeshaje? Chukua hatua.