Bwana huyo, Kevin Gaylor wa Colorado Springs Marekani, alikutana na msichana kwenye mtandao wa Craiglist.com na kumwambia aende kumtembelea nyumbani kwake. Hata hivyo mke wa bwana Kevin alirudi nyumbani ghafla, na kumfaya bwana huyo kupagawa asijue la kufanya.
Muda mfupi baada ya mke wake kuwasili, msichana aliyealikwa naye akafika. Kujaribu kuokoa jahazi bwana huyo alipiga simu polisi na kusema kuna mwizi nyumbani kwake. Gazeti la Metro limesema polisi watano walikwenda haraka nyumbani kwa bwana Kevin kupambana na mwizi ambaye waliambiwa alikuwa na silaha.
Badala yake polisi walikuta msichana mwenye umri wa miaka 20 akiwa nje ya nyumba ya bwana Kevin. Msichana huyo aliwaambia Polisi kuwa alisafiri kwa muda wa zaidi ya saa moja ili kukutana na Kevin, na kuwa walikuwa wakiwasiliana kwa muda wa wiki mbili kupitia simu na internet. Polisi walipogonga mlango wa bwana Kevin, alitoka na kuanza kuzungumza kwa sauti ya chini na kuwasihi polisi wamuondoe msichana huyo. Hata hivyo bwana huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa polisi.