Mtanzania aliyekamatwa Kenya akidaiwa kufanya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa uliosababisha vifo vya watu 148, Rashid Charles Mberesero (20) ni mwanafunzi wa kidato cha tano, lakini uongozi wa shule anayosoma umesema alitoweka shuleni hapo Desemba Novemba 2014.
Habari
zilizothibitishwa na wazazi wake ni kuwa mwanafunzi huyo anasoma katika
Shule ya Sekondari ya Bihawana, Dodoma, baada ya kufaulu katika Shule
ya Sekondari Gonja mkoani Kilimanjaro.
Mama mzazi wa
kijana huyo, Fatuma Ali alisema jana kuwa: “Baada ya kufaulu
alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Bihawana na likizo alirudi
nyumbani na baada ya likizo kuisha aliniaga anarudi shuleni.”
Taarifa
hizo zimekuja wakati Mberesero maarufu kwa jina la Rehani Dida,
akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Nairobi baada ya watuhumiwa
wengine kufikishwa mahakamani juzi.
Mwendesha
mashtaka, Daniel Karuri alisema, “Rehani Dida” hakufikishwa kortini
kwani alikuwa na wapelelezi mjini Garissa kukusanya ushahidi zaidi,
baada ya kukiri kuwa ni mfuasi wa kundi la Al-Shabaab.
Mtanzania
huyo anadaiwa kukamatwa baada ya kujificha kwa saa nane akiwa
amejichanganya na maiti, lakini baadaye alipanda na kujificha darini
akiwa na mabomu.
Kauli ya wazazi
Jana,
mama huyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa haelewi ni nani aliyemshawishi
mwanaye kujiunga na kundi hilo na kwamba jambo hilo limemshtua.
“Hizi
taarifa tumezisikia na kuona kwenye TV na kwa kweli zimetushtua sana,
mimi nahisi huko shule ndiko alikokutana na watu wabaya,” alisema Fatuma
ambaye ni mkazi wa Gonja wilayani Same.
Baba mzazi wa
mtuhumiwa huyo, Charles Mberesero Temba, alikiri kuwa Rashid ni mtoto
wake ambaye alizaa na Fatuma mwaka 1994 na miaka yote alikuwa akiishi na
mama yake.
“Huyo mtoto sijawahi kuishi naye, muda wote
tangu 1994 alikuwa akilelewa na mama yake,” alisema Temba na kuongeza
kuwa hakuwahi kuishi na mzazi mwenzake huyo.
“Mwaka
jana mama yake ndipo alinikutanisha na mtoto na akanitambulisha na mimi
nikamshauri abadili dini kwa sababu mimi ni Mkristo Mkatoliki,” alisema.
Alisema
aliendelea kuwasiliana naye na aliwahi kumpeleka kanisani mara tatu
akimshauri abadili dini ili arudi kwenye dini ya baba, lakini alikataa.
Alisema
inavyoonekana ushauri wake huo haukupokewa vizuri na mwanaye na huo
ndiyo ulikuwa mwanzo wa mawasiliano baina yao kukatika.
Kutoka Bihawana
Habari
zilizopatikana jana kutoka shuleni Bihawana zilisema kuwa Mberesero
alitoroka shuleni Novemba mwaka jana, baada ya kukaidi kuvua kofia
katika eneo la shule.
Mkuu wa Shule hiyo, Joseph
Mbilinyi alisema alimpokea mwanafunzi huyo Agosti 15, mwaka jana
akitokea katika Shule ya Sekondari ya Kigwe wilayani Bahi.
Alisema
mwanafunzi huyo alipata uhamisho baada ya kubadilisha masomo kutoka
masomo ya sanaa mchepuo wa Historia, Jiografia na Kiswahili (HGK) na
kuingia katika masomo ya sayansi ya Fizikia, Kemia na Biolojia (PCB).
Mbilinyi
alisema katika shule hiyo wanafunzi walikuwa na mazoea ya kuvaa rozali
na kofia, jambo ambalo alilipiga marufuku lakini Novemba 24, mwaka jana
alikutana na kijana huyo akiwa amevaa kofia.
“Nilimwambia
aivue aichanechane mbele yangu, lakini alikataa na kunijibu kuwa
amezoea kuivaa na hawezi kuichana.
"Kwa sababu ilikuwa ni usiku niliondoka na kofia hiyo na kumwambia kesho yake asubuhi aje ofisi kwangu ili tumalize suala hilo, alikuwa ni mtu wa kwanza kufika ofisi kwangu.
"Nilimwambia anieleze kwa nini hataki kuichana, ningeweza kumsaidia kumtafutia shule ambazo zinaruhusu mavazi hayo.”
"Kwa sababu ilikuwa ni usiku niliondoka na kofia hiyo na kumwambia kesho yake asubuhi aje ofisi kwangu ili tumalize suala hilo, alikuwa ni mtu wa kwanza kufika ofisi kwangu.
"Nilimwambia anieleze kwa nini hataki kuichana, ningeweza kumsaidia kumtafutia shule ambazo zinaruhusu mavazi hayo.”
Alisema
hata baada ya mazungumzo hayo, Rashid hakueleza kwa nini alikataa
kuichana ndipo alipoambiwa kuwa angerejeshwa nyumbani ili aje na mzazi
wake na aichane mbele yake.
“Kwa kawaida wanafunzi
wengine ukiwaeleza hivyo, huwa wanaomba msamaha yanaisha lakini kwa
Rashid ilikuwa ni tofauti, aliniambia yuko tayari kurudishwa nyumbani
lakini siyo kuchana kofia hiyo,” alisema.
Mwalimu huyo
aliongeza: “Niliona njia ya kumsaidia ni kuwashirikisha walimu ambao
wanasimamia msikiti wetu huu. Walimu walimuita na akakubali kupewa
adhabu ili jambo hilo liishe bila kufikishwa kwa wazazi wake.”
Hata
hivyo, alisema baada ya mazungumzo hayo, Rashid alichukua begi lake na
kuondoka kwenda mjini na kuwaacha wenzake wakimalizia mtihani wa
Biolojia.
“Nilipata shida sana sikupenda mwanafunzi
huyu aondoke shuleni, nilitaka hili jambo lipate suluhu. Nilipigia simu
alizoandikisha shule ikiwamo ya baba yake bila mafanikio kwa sababu
hazikupokewa, isipokuwa moja ambayo ilipokelewa na mwanamke ambaye
alikana kumfahamu.
“Hadi leo bado ni mwanafunzi wetu
kwa sababu kanuni zinasema baada ya siku 90 kama mwanafunzi hajaonekana
shuleni, tunapeleka jina kwenye Bodi ya Shule ambayo itatoa uamuzi,”
alisema.
Katibu mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi
Waislamu katika shule hiyo, Mungi Ramadhan Mungi alisema Rashid alikuwa
ni mtu wa msimamo, akitaka jambo lake hata kama halina usahihi
analisimamia.
“Aliwahi kutaka kupigana msikitini mara
mbili, mara ya kwanza tulikuwa tukiuliza maswali kuhusu masomo ya
darasani yeye akasema hairuhusiwi kufanya hivyo msikitini,” alisema.
Alisema hatua hiyo ilizua mabishano na alifikia uamuzi wa kutaka kuwachapa walioongelea mambo ya masomo ndani ya msikitini.
“Alikuwa
ni mtu wa msikitini na bwenini mara nyingi hakupenda kuchanganyika na
wenzake, jambo hilo lilimfanya hata kukosa marafiki,” alisema.
Alisema aliwahi kuwahadithia kuwa alibadili dini akiwa anasoma sekondari huko Moshi.
Mwalimu
anayewasimamia wanafunzi wa Kiislamu, Mohamed Mwijuma alisema baada ya
Rashid kutoroka shuleni hapo waligundua alikuwa ni mwanafunzi aliyekuwa
na matumizi yasiyo ya kawaida.
“Pia tuligundua kila
mwisho wa wiki alikuwa akitoroka kwenda mjini,” alisema Mwijuma ambaye
alishiriki kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la kukutwa na kofia shuleni.
Hata hivyo, alisema Februari mwaka huu, Rashid alirejea mwisho wa wiki na kuondoka moja kwa moja na mizigo yake yote.
Habari
zilizopatikana shuleni hapo zilisema baada ya Rashid kutajwa kuhusika
na tukio hilo, mama yake mzazi alifika shuleni hapo kumtafuta mwanaye.