Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
wakati dunia bado ikiwa na kumbukumbu mbaya ya ndege ya shirika la ndege
la Ujerumani na vifo vya abiria 150 ndaniye,kituko kingine kimegubika
tasnia ya urubani baada ya marubani wawili kuondolewa kwenye zamu ya
urushaji ndege kufuatia madai ya wawili hao kuzikunja katika chumba cha
kuongozea ndege.
Marubani hao hurusha ndege za shirika la ndege la
India, Air India walishushwa katika ndege yao baada ya rubani msaidizi
kumshambulia captain wake ama nimwite rubani kiongozi .Hata hivyo ili kulinda hadhi ya shirika la ndege la India, maafisa wa juu wa shirika hilo walidai kuwa marubani hao wawili walirushiana maneno na hawakuingiana mwilini.
Msemaji wa shirika hilo la ndege amedai kwamba marubani hao wawili wote waliondolewa kwenye zamu zao na maswali tele yaligubika msuguano wa marubani hao,na kitengo cha nidhamu cha shirika hilo la ndege kilipewa jukumu mara moja kuwaketisha marubani hao kujua chanzo cha sintofahamu hiyo na hatimaye kuyamaliza.
Lakini askari wa ngazi za juu nchini India wamedai kwamba chanzo cha mzozo huo kilianzia pale Rubani kiongozi alipomtaka rubani msaidizi kurekodi mwenendo wa ndege hiyo ikiwemo idadi ya abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo kabla haijaanza safari yake.