Habari
wasomaji wangu wa Abdallahmagana.com , munaoendelea kuperuzi, Leo ni
Aprili Mosi, ambapo kila mwezi wa nne tarehe moja kama ya leo Duniani
kote watu mbalimbali huifaanya siku hii kama ni ya kutaniana na kufanya
jambo la mzaha ama ujinga ambalo ufanywa kuanzia tarehe inapoanza hadi
saa nne asubuhi.
Hata
hivyo siku hii ya wajinga kwa kipindi hiki imezidi kuwa na nguvu hasa
baada ya kuongezeka mitandao ya kijamii ambayo watu mbalimbali
wanaooitumia kutumia wasaha wa kuposti taarifa za uongo na uzushi huku
wengine wakienda mbali na haataa kubandika picha za ku-edit ilimradi tu
aonekane ni mkweli.
Hatahivyo
wapo wanaofanya hivi pasipokujulisha mwisho wa taarifa yake hiyo kama
ni siku ya wajinga na wapo wanaofanya hivyo kuajulisha ni siku ya
wajinga na mambo kama hayo.
Mtandao
huu tunakuletea makala maalum ambayo inaelezea siku hiyo wa wajinga
duniani ambayo pia imeelezea na namna na suala la kiimani inavyoweza
kuwa baya. .
Uzushi na Maovu
بسم الله الرحمن الرحيم
BismiLLaah
walhamduliLLaah Rabbil ‘Aalamiyn. Was-Swalaatu was-Salaamu
‘alaa Nabbiyihi asw-Swaadiq Al-Amiyn, wa ‘alaa aalihi wa Swahaabatihi
al-Ghurr Al-Mayaamiyn, wa man Tabi’ahum bi Ihsaani ilaa Yawmid Diyn.
Amma ba’ad:
ASILI YA APRIL FOOL
Asili ya April Fool haikujulikana kwa uhakika na kuna rai mbali mbali zinazohusiana nayo.
Wengine wamesema imeanza kutokana na sherehe za majira ya kuchipua (Spring) katika ikwinoksi (siku ya mlingano) tarehe 21 Machi.
Wengine
wamesema kuwa huu ni uzushi uliochomoza France mwaka 1564 M, baada
ya utangulizi wa kalenda mpya. Wakati mtu alipogoma kukubali kalenda
mpya akaishia kuwa ni mwathirika wa baadhi ya watu ambao wamemsababisha
aathirike kufedheheka na wakamfanyia istihzai na kumtania, akawa ni
kichekesho kwa watu.
Wengine
wanasema kuwa uzushi huu umeanza asili yake katika nyakati za kale na
sherehe za mapagani zilikuwa na uhusiano na siku hasa mwanzo wa majira
ya kuchipua. Kwa hiyo hii ni kasumba ya ibada za mapagani. Inasemekana
kuwa nchi nyingine, kuwinda hakukufaulu siku za mwanzo za uwindaji.
Le poisson d’avril (Samaki wa Aprili)
Wazungu
wameiita April Fool kwa jina la ‘le poisson d’avril’ (Samaki wa
Aprili). Na sababu hii ni kutokana na jua linavyosogea kutoka nyumba ya
zodiaki (nyota za unajimu) ya Pisces (Nyota ya samaki) ikielekea nyumba
nyingine. Au kwa sababu ya neno la poisson ambalo maana yake ni samaki,
hivyo ni ugeuzaji wa neno la ‘passion’ ambayo ina maana ya ‘kuteseka’.
Kwa hiyo ni alama ya kuteseka aliyovumulia Nabii ‘Iysa (Alayhis Salaam)
kama walivyodai Wakristo. Na madai yao haya yalitokea wiki ya kwanza
katika mwezi wa April.
Baadhi
ya makafiri wameiita siku hii ‘Siku nzima ya wajinga’ kama
inavyojulikana Kingereza. Hii ni kwa sababu uongo wanaousema ili wale
wanaousikia waamini kwa hiyo wanakuwa ni waathirika wa wale
wanaowafanyia dhihaka.
Utajo
wa mwanzo kabisa kwa Lugha ya Kingereza ilikuwa ni katika gazeti la
Dreck. Siku ya pili ya Aprili 1698 M, gazeti hili lilitaja kwamba idadi
kadha ya watu walialikwa kuhudhuria uoshaji wa watu weusi katika mnara
wa London asubuhi ya siku ya mwanzo ya Aprili.
Tukio
maarufu kabisa lililotokea Ulaya tarehe 1 Aprili lilikuwa wakati gazeti
la Kingereza ‘Evening star’ lilipotangaza mwezi wa Machi 1746 M kwamba
siku ya pili tarehe 1 Aprili, kutakuwa na gwaride la punda mji wa
Islington Uingereza. Watu wakakimbilia kuwatazama wanyama hao na
kulikuwa na zahma kubwa. Wakaendelea kusubiri na walipochoka kusubiri,
waliuliza kutaka kujua hili gwaride litakuweko baada ya muda gani.
Hawakupata jibu, hivyo wakatambua kuwa wamekuja kufanya maonyesho yao
wenyewe kama kwamba wao ndio mapunda.
Mmoja
wao ameandika kuhusu asili ya uzushi huu kwa kusema: Wengi wetu
tunasherehekea siku inayojulikana kuwa ni April Fool, au ikiwa
itafasiriwa kihalisi ‘Siku ya Ujanja’. Lakini je, tunajua siri chungu
inayohusikana na siku hii?
Habari nyingine ambazo usahihi wake umetiliwa shaka na wanahistoria ni kuwa:
Waislamu
walipotawala Hispania (Spain) takriban miaka elfu iliyopita, kulikuwa
na nguvu kubwa ya utawala wa Kiislam ambayo haikuwezekana kuivunja.
Wakristo wa Kimagharibi walitamani kuufuta Uislamu katika mgongo wa
ardhi na walifaulu kwa kiwango fulani.
Walijaribu
kuzuia Uislamu kusambaa Hispania na walitaka kuuzima na wautoweshe
kabisa lakini hawakufaulu, ingawa walijaribu mara nyingi bila ya
kufaulu.
Baada
ya hapo, makafiri walituma majasusi Hispania kufanya utafiti ili kujua
siri ya nguvu za Waislamu ambayo haikuwezekana kuishinda. Wakatambua
kuwa kushikamana na Taqwa (Ucha Mungu) ndio sababu.
Wakristo
walipotambua siri ya nguvu za Waislamu, wakaanza kufikiria mikakati za
kuvunja nguvu hiyo. Na kwa ajili hii wakaanza kupeleka ulevi na sigara
bure huko Hispania.
Mbinu
hizi kwa upande wa Magharibi zilifaulu kuleta taathira na imani za
Waislamu zikaanza kulegea, hasa miongoni mwa vizazi vipya Hispania.
Matokeo yake ni kwamba Wakristo Wakatholiki waliikandamiza Hispania
nzima na wakauangamiza utawala wa Kiislamu katika ardhi hiyo,
utawala ambao ulidumu zaidi ya miaka mia. Ngome ya mwisho ya Waislamu
Grenada ilianguka tarehe 1 Aprili, hivyo wakaichukulia kuwa ni ‘Siku ya
Ujanja ya Aprili’ au ‘Siku ya Wajinga ya April’. Ujanja kwa wale
walioufanya, na Ujinga kwa wale waliofanyiwa na kutumbikia ndani yake.
Tokea
mwaka huo hadi sasa, wanasherehekea siku hii na wanachukulia kuwa
Waislamu ndio wajinga. Hawakuuhusisha ujinga huu na jeshi la Granada
pekee kuwa ni wajinga, bali wamekusudia kuwa ni Umma wa Kiislamu mzima
kuwa ni wajinga.
Hata
hivyo, habari hizi tumezinukuu hapa kwa kuwa zimeenea sana miongoni wa
Waislam, lakini kama tulivyotangulia kueleza, ni kuwa, uhakika na ukweli
wake una mashaka kwa sababu kuna wanaosema kuwa wakati huo sigara na
uvutaji tumbaku ulikuwa haujaanza hadi baada ya kushindwa Waislamu huko
Hispania. Wahahistoria wanasema sababu za kushindwa Waislamu zilikuwa ni
wenyewe kujiingiza zaidi kwenye mapenzi ya kidunia na starehe, pamoja
na kuacha mafundisho sahihi ya Uislam na badala yake kuchanganya zaidi
na falsafa ya Kigiriki na kutegemea zaidi fikra za kirumi katika
kuendesha mambo yao badala ya mwongozo imara wa Kiislam. Kadhalika kuna
Waislamu waliokuwa wakishirikiana na makafiri katika kupambana na
makundi mengine ya Kiislam waliyokuwa hawaelewani nayo kama tunavyoona
leo hii.
BAADHI YA UDANGANYIFU WANAODANGANYANA WATU KATIKA
SIKU HII YA APRIL FOOL
Wengine
wanapewa habari ya mmoja wa kipenzi chake katika familia kama mtoto,
mke au mume kwamba amefariki na kwa wengine taarifa hizo husababisha
hata kifo chao kutokana na kutokustahamili kupata mshtuko huo. Wengine
wanapewa habari ya kufukuzwa kazi, au kuwashtua kwa habari mbaya kama
kuunguliwa moto nyumba yake, au familia yake kupata ajali, na
husababisha aathirike mtu kwa mshtuko huo hadi apate maradhi ya moyo, au
maradhi ya kupooza au hata kifo cha ghafla.