TUKIO la aina yake! Dereva wa bodaboda aliyejulikana kwa jina la Alex Wilson amekutwa ameuawa kwa kuchinjwa na kuporwa pikipiki lakini cha ajabu, siku ya mazishi yake kaburini kukazikwa mgomba baada ya mwili kuzuiwa usizikwe, Uwazi limechimba kisa kamili.
Inadaiwa kuwa, katika kutafuta alikokuwa akiishi marehemu huyo, wenzake walifanikiwa kupapata na kumkuta mtoto wa mama mwenye nyumba ambapo walimuonesha picha za enzi za uhai wa Alex naye ndugu huyo alikiri kwa kusema ni kaka yake.
Walimuuliza mtoto huyo aliko mama yake akasema yuko safarini Sumbawanga kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.
“Tulimwomba namba ya simu ya mama yake, akatupa. Tulipompigia alisema kweli anamtambua marehemu lakini yeye yuko Sumbawanga,” alisema mmoja wa madereva bodaboda hao.
“Siku iliyofuata, yaani Aprili 9, mwaka huu, tukiwa na baadhi ya ndugu wa mbali wa Alex tulikwenda Kituo cha Polisi Afrikana (Dar) kuomba kibali cha mazishi, lakini ikabidi polisi wafanye mawasiliano na yule mama aliye Sumbawanga.
“Polisi walimpigia simu na kuweka loud speaker (spika kwa sauti ya nje) wakimtaka mama huyo afike Dar haraka kwa mazishi ya mtoto wake au waruhusu mtoto wake azikwe.“Lakini yule mama alijibu kuwa, wasijaribu kufanya kitendo chochote cha mazishi kwa vile anajua kuwa mwanae huyo hajafa na anajua alipo.
Baada ya hapo bodaboda hao kwa kushirikiana na ndugu wa mbali, walilazimika kukata mgomba na kuuzika kaburini badala ya mwili wa marehemu.Mgomba huo ulizikwa katika Makaburi ya Kinzidi, Aprili 9, mwaka huu kwa kile kilichodaiwa kuwa, kuacha kaburi wazi wakati lilishachimbwa kwa ajili ya maziko ni uchuro kwa wengine walio hai.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na marehemu Alex, mwanamke huyo alisema:
“Ni kweli Alex namfahamu na tulifahamiana Dar es Salaam na hii ni kutokana na kunifahamu mimi ni mtu wa Sumbawanga hivyo siku za nyuma alikuja nyumbani kwangu na kujitambulisha, mimi nilimchukulia kama mwanangu.